• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
MITAMBO: Kisiagi cha kuongeza thamani ya uyoga

MITAMBO: Kisiagi cha kuongeza thamani ya uyoga

NA RICHARD MAOSI

WAKULIMA wanashauriwa kujifunza namna mbalimbali za kukausha ama kuweka uyoga katika mazingira baridi ili kuhifadhi kwa muda mrefu.

Hii ni kwa sababu uyoga ni mojawapo ya vyakula vilivyojaa virutubishi muhimu vya calcium, amino acids na protini.

“Kilimo cha uyoga ni rahisi na mkulima anaweza akavuna na kuuza moja kwa moja sokoni au kutumia nyumbani,” anasema Paul Nyongesa mkulima wa uyoga aina ya oyster na button kutoka Kaunti ya Kakamega.

“Pia unaweza kuongezea thamani kwa kukausha na kuuza baadaye,” anaongeza.

Akilimali ilitaka kujua ni vipi wakulima wa uyoga hukabiliana na hasara, hususan bidhaa zao zinapokosa soko.

Nyongesa anasema kuwa mkulima anahitaji vifaa vikubwa kuhifadhi zao hilo kutokana na uzalishaji mkubwa wa uyoga uliopo nchini.

Kiwango hiki cha juu cha mazao sokoni hufanya bei ya uyoga kudorora na mazao mengi kuharibika, kwani uyoga huchukua siku tatu tu kuanza kuoza baada ya kuvunwa.

Mtambo wa kusaga

Njia ya kutunza uyoga wako ni kupitia uongezeaji thamani ambapo zao hilo hugeuzwa bidhaa mbalimbali za kudumu.

Mtambo wa Simple Milling Machine husaidia pakubwa kusaga uyoga ili kuugeuza unga unaodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Hakikisha uyoga umekomaa la sivyo unaweza kuwa na ukungu, ambao si salama kwa matumizi ya binadamu.

Alice Wamboi kutoka Kaunti ya Kiambu anaeleza kuwa, taratibu za kukausha uyoga hutegemea majira ambayo mkulima amevuna.

Kwa kawaida uyoga huchukua muda mrefu kukauka hasa msimu wa baridi, kinyume na siku za kiangazi ambapo huhitaji siku tatu hivi kupoteza unyevu.

Wamboi anasema uyoga unapovunwa hukatwa na kutandazwa juu ya karatasi safi.

Aidha, baadhi ya wakulima hutumia aina maalum ya draya za sola.

Katika siku tatu hizo uyoga hupata ugumu ishara tosha kuwa unyevu umekwisha.

Wamboi huuchukua na kuweka ndani ya kisiagi hicho na kutengeneza unga.Uyoga uliokaushwa na kusagwa kando na kudumu pia huwa na bei ya juu.

Huuzwa Sh200 kwa gramu 40, ikilinganishwa na uyoga wa kawaida ambao huuzwa Sh150 kwa gramu 125.

Iwapo unataka kutumia uyoga freshi unaweza kuhifadhi ndani ya jokofu.

Nyongesa anasema kuwa uyoga wa namna hii unaweza kudumu kwa kati ya siku 10-12, kwani mara nyingi matumizi yake huwa ni ya nyumbani tu.

Kuandaa unga wa uyogaWamboi anashauri kuwa pindi uyoga unapotolewa shambani husafishwa ili kuondoa vumbi, mchanga na mategu mengine.

Kisha hukatwa vipande vipande na kukaushwa juani ama kutumia draya ya sola.

Baadhi ya uyoga hupakiwa na mwingine kusagwakuwa unga.

Unga huu umebainika kuwa chakula bora kwa watoto, wazee na wanaogua maradhi sugu kama shinikizo la juu la damu au maradhi ya moyo.

Utunzi wa mtamboIli kisiagi kifanye kazi vyema na kudumu, mkulima anatakiwa kukisafisha kila wakati na kupaka rangi ili kuzuia kutu.

Pili, noa meno ya mashine hiyo ili kuimarisha makali yake kwa wepesi.

Kulingana na Alice anasema kuwa njia ya jadi ambayo imekuwa ikitumika kukausha uyoga ni ile ya kuanika kwenye jua.

Ila mkulima hakuwa na namna ya kudhibiti nzi, vumbi wala uchafu hususan katika hatua ya mwisho ya usindikaji ambayo ni kutwanga ilmuradi kutengeneza unga wa uyoga.

Hata hivyo anasema kuwa siku hizi kuna aina tofauti za uyoga, ambapo kila uyoga una ladha yake.

Lakini kabla ya kutumia mtambo wa milling machine kuongeza thamani utaratibu huu hufuatwa. Katika hatua ya kwanza anasema mkulima anapaswa kusafisha uyoga ili kuondoa vumbi, mchanga na mategu mengine ambayo huondolewa kwa kutumia brashi.

Kuanzia hapo anapaswa kutenganisha sehemu kwa kukata na kuzitupa sehemu zilizoharika, akabakia na uyoga safi, kisha baadaye uyoga hulowekwa ndani ya maji na hatimaye kukatwa vipande.

Anasema wakati wa usindikaji uyoga hupangwa ukiwa umekauka na kuingizwa ndani ya mtambo wa milling machine.

Aidha uyoga unaweza kuchanganywa na aina nyingine ya nafaka kama vile mtama na shayiri ili kutengeneza unga uliokolea virutubishi zaidi.

Anaeleza katika hatua hii mkulima anaweza kuongeza chumvi kwenye mchanganyiko wake, ikizingatiwa kuwa mtambo wa milling machine una mfumo maalum wa kusawazisha na kunogesha ladha.

Katika kipindi cha dakika 10 hivi uyoga uliokaushwa huwa umebadilika na kuwa ungaunga.

Kutokana na mseto huu Alice huuza uyoga wake kwa wamiliki wa mikahawa, ambayo hutumia uyoga kuandaa mchuzi.

Baadhi ya wauzaji hupakia uyoga na kuwauzia wafanyibiashar wengine.

You can share this post!

NJENJE: Kenya kuagiza ngano kutoka Serbia kuziba pengo...

Mvinyo, juisi na jemu ya mtama kutoka JKUAT

T L