• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 3:36 PM
MITAMBO: Mashini kusaidia kilimo endelevu kulinda mazingira

MITAMBO: Mashini kusaidia kilimo endelevu kulinda mazingira

NA RICHARD MAOSI

UTUMIZI wa mbinu bora za kuandaa shamba msimu wa upanzi, huwasaidia wakulima kuboresha udongo, rutuba na viumbe hai mchangani.

Bi Millicent Obonyo ambaye ni mkulima wa viazi tamu na mihogo kutoka Kaunti ya Machakos, anasema kuwa mimea yake huwa na mizizi mirefu na inambidi kulainisha udongo kwanza kabla ya kupanda ili mizizi yake iweze kufikia unyevu katika kina kirefu.

Pili, anasema udongo uliolainishwa hupunguza gharama ya ukulima ikilinganishwa na kupanda kwa kawaida, kwa sababu trekta ya mkulima inaweza kutumia kiasi kidogo cha mafuta katika ardhi laini.

“Pia inawezekana kuendesha kilimo chenye natija kwa kutunza udongo wa juu katika shamba, kwa kupunguza mmomonyoko wa udongo hasa kasi ya maji inayosababishwa na mvua,” asema.

Aidha hii huja na faida nyinginezo nyingi ikiwemo ni pamoja na kuboresha uhai wa udongo, hivyo basi kuleta mazingira mazuri kwa mbegu kukua au kuota.

Kwa muda kirefu upanzi wa mimea kwa kutumia majembe ya kawaida kumekuwa kukichangia katika uharibifu wa udongo, virutubishi na kukatiza ghafla maisha ya viumbe hai .

Baadaye matokeo ni kuwa udongo hubaki wazi sana kiasi kwamba ni rahisi kubebwa na upepo au maji ya mvua.

Hii ndio maana kumevumbuliwa mtambo unaojulikana kama Sisaw Plough ili kuwasaidia wakulima kuendesha kilimo cha kutunza mazingira.

Kilimo cha kutunza mazingira kinaweza kufanya vyema wakati ambapo mkulima atakuwa ameyafikia mahitaji yote ya afya ya udongo kama kutunza viumbe hai udongoni.

Mhandisi wa kilimo, Bi Maureen Wambui kutoka Shamba la Marula eneo la Naivasha, anasema kuwa ukosefu wa mashini kama hizi ndio kizingiti kikubwa kwa ufanisi wa wakulima.

“Ukosefu wa elimu ya sayansi ya udongo pia unaathiri uendeshaji wa kilimo endelevu,” anaeleza.

Anaeleza Akilimali kuwa mashini hiyo hutumika mara nyingi kuendesha kilimo katika kipande kikubwa cha ardhi sehemu ambazo mkulima atakuwa akipanda aina mbalimbali ya mazao.

Ni mashini ambayo hutumika kulima kina kirefu cha ardhi kwa kusawazisha udongo.

Mashini hiyo anaeleza kuwa hutumika kupindua udongo na kuhakikisha kuwa viumbe hai udongoni pia vinalindwa.

Mashini yenyewe imeundwa kwa chuma kizito ingawaje kina uwezo wa kupenya ardhini .

“Mtambo huu unaweza kupenya hadi sentimita 40 ardhini, hali ambayo husaidia kutengeneza njia mbadala kwa michirizi ya maji na mizizi ya mimea kupenya.”

Kwa upande mwingine, Wambui anasema kuwa mtambo huu unaweza kumsaidia mkulima kutunza hadi asilimia 40 ya unyevu unaopatikana kwenye udongo.

Pia uwezo wa mimea kuota huongezeka kati ya asilimia 15-20.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Mradi wa chuo kuwafaa wakulima wa Migori

UJASIRIAMALI: Anahesabu mabunda ya noti kwa kuunda vinyago...

T L