• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 12:42 PM
ZARAA: Mradi wa chuo kuwafaa wakulima wa Migori

ZARAA: Mradi wa chuo kuwafaa wakulima wa Migori

NA LABAAN SHABAAN

SHADRACK Otieno Obura ni mkulima wa mtama ambaye amenufaika na miradi ya majaribio ya kilimo unaoendelezwa na idara ya kilimo ya Chuo Kikuu cha Rongo.

Obura, aliyeanza kilimo mwaka wa 1997, anaendeleza kilimo cha mimea mbalimbali kama vile ndizi, mahindi, miti, miche, mihogo, mtama na ufugaji ng’ombe katika shamba lake kijijini Ng’iya, Suna Mashariki Kaunti ya Migori.

“Nafurahi kwa sababu Chuo Kikuu cha Rongo kilinitafuta kunishirikisha katika mradi wa upanzi wa mtama ambao unaninufaisha kupata chakula na kuwasaidia katika utafiti wa mimea,” Obura anaambia Akilimali.

Kwa mujibu wa Obura, Chuo Kikuu cha Rongo kilimhusisha kwa sababu yeye ni mmoja wa wakulima mashuhuri eneo la Migori na huwa na uhusiano na mtandao mkubwa wa wakulima wanaomtegemea kwa mafunzo.

Obura anasifia umuhimu wa mtama kwa afya na biashara. Katika shamba lake la mtama la nusu ekari tayari wateja wamejisajili kununua hata kabla ya kuvunwa kwa kuwa kuna mahitaji makubwa ya zao hili.

“Mimi huuza kilo mbili ya mtama kwa Sh150. Baada ya kuvuna mamia ya kilo, mimi hutenga mavuno ya kutumia nyumbani na mbegu na yanayobaki nauza kwa majirani. Sina shida ya soko, wateja hununua wakati wa mavuno,” Obura anaeleza.

Mkulima huyu anaarifu kuwa uvumilivu wake ndio umemdumisha shambani pamoja na tajiriba yake katika kilimo cha mtama licha ya wakulima eneo hili kuacha kwa sababu ya ndege wanaovamia mashamba ya mtama.

Kutumia maarifa aliyopata kutoka kwa wataalamu wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Rongo, Obura anajua kudhibiti ndege kwa kuwawinga wakati mwafaka.

Kwa sababu ya uzoefu, amejua ndege huja shambani mara mbili kwa siku; asubuhi na jioni.

Baina ya safu za mimea ya mtama kuna kamba zinazoning’inia na kumetameta. Kamba hizi hutoa sauti upepo unapovuma na hufukuza ndege. Iwapo hakuna upepo, Obura huhakikisha yuko shambani wakati mwafaka kufukuza ndege kwa kuwapura mawe.

“Ijapokuwa tunajua tunafaa kuvuna baada ya miezi mitatu ama minne, ndege kuvamia mashamba ni ishara kuwa ni msimu wa mavuno. Huu ndio wakati sisi hukaa shambani kupunguza kupoteza mavuno kwa ndege waharibifu,” Obura anasema.

Kila baada ya msimu wa mavuno Obura anahitajika kupanda mmea mwingine kwenye kipande alichopandia mtama ili kudhibiti magugu na magonjwa kama anavyoshauriwa na wataalamu wa kilimo.

Kwenye shamba lake kuna aina mbalimbali ya mtama zinazotumika kufanyia utafiti unaolenga kustawisha utoshelevu wa chakula nchini.

Kulingana na Shirika la Utafiti wa mimea na mifugo Kenya (KALRO) mtama aina ya finger millet una mahitaji makubwa miongoni mwa wakenya. Kwa hivyo mmea huu unaweza kumpa mkulima faida kubwa.

Mtama hukuzwa sanasana katika maeneo ya Magharibi, Nyanza na Bonde na Ufa.

Kulingana na KALRO, wanasayansi na wakulima Magharibi ya Kenya wametambua aina mbili za mtama zinazonawiri na kuvutia mapato makubwa.

Aina hizo ni P-224 and Gulu-E na zinapendekezwa sehemu za baridi na zenye mvua kidogo. Aina hizi za mtama hustahimili magonjwa na hukomaa haraka.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Siri yake ni bidii shambani na kusaka wateja...

MITAMBO: Mashini kusaidia kilimo endelevu kulinda mazingira

T L