• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Mitambo na mashine kuboresha kilimo 

Mitambo na mashine kuboresha kilimo 

NA SAMMY WAWERU

HUKU athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea kuonyesha makali yake, mifumo ya teknolojia kuendeleza kilimo inapigiwa upatu. 

Mosi, wakulima wanashauriwa kukuza mbegu zilizoimarishwa kiteknolojia na zenye ustahimilivu wa hali ya juu kwa ukame, wadudu na magonjwa ibuka ya mimea.

Wanasayansi na watafiti katika utandawazi sekta ya kilimo, wanajibidiisha kuvumbua na kuunda mbegu hizo.

Kenya ikiwa miongoni mwa mataifa matatu Upembe wa Afrika yaliyolemewa na athari za mabadiliko ya tabianchi, 2022 ni mwaka wa tatu mvululizo kushuhudia janga la ukame.

Nchi nyingine ni Somalia na Ethiopia.

Mimea, malisho ya mifugo imekauka kufuatia upungufu na ukosefu wa mvua, mifugo wakiishia kufa njaa.

Kwa sasa, serikali inaongoza oparesheni na kampeni kusambaza chakula cha msaada maeneo kame (ASAL).

Zaidi ya kaunti 29 zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na ukame, hali inayoshuhudiwa ikitajwa kuwa mbaya zaidi katika historia ya Kenya.

Katika muktadha huohuo wa teknolojia kufanikisha shughuli za kilimo, mashine na mitambo ya kisasa ni nguzo muhimu kuepushia wakulima hasara msimu wa mavuno.

Zipo mashine tumbi nzima zinazotumika kuvuna mazao shambani, zilizovumbuliwa na nchi zilizoimarika kilimo.

Mfano, Japan, China, Uingereza na Amerika, mataifa hayo yakiwa machache tu kutaja yamekumbatia matumizi ya mashine, kuanzia upanzi, palizi, upuliziaji dawa, unyunyiziaji maji, na uvunaji.

Kando na kuboresha mazao, zinapunguza gharama.

Baadhi ya mashine hizo, hasa za upanzi, dawa na mavuno zimetua nchini.

Ngano, ni kati ya nafaka zinazonufaika kupitia mashine za kuvuna maarufu kwa Kiingereza Combine Harvester.

“Changamoto zinazotokana na tabianchi, matumizi ya mitambo, mashine na teknolojia za kisasa ndio suluhu,” asema Mwenyekiti Muungano wa Maonyesho ya Kilimo Nchini (ASK) tawi la Nairobi, Bw Joseph Mugo.

Sehemu zinazozalisha ngano nchini, kama vile Nakuru, Narok, Laikipia, Uasin Gishu, na Trans Nzoia, wakulima wanatumia mashine kuvuna mazao.

“Kinyume na miaka ya kitambo ambapo tulikuwa tunavuna ngano kwa mikono, kupitia mashine hasara ya mavuno imepungua kwa kiasi kikuu,” aelezea John Koech, mkulima wa ngano Eldoret.

Ngano huvunwa mazao yanapokauka. 

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Sadio Mane kubeba Senegal...

TAHARIRI: Hazina ya Hasla: maoni ya wananchi yapewe uzito

T L