• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 3:09 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Sadio Mane kubeba Senegal mabegani jinsi alivyofanya El Hadji Diouf 2002

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Sadio Mane kubeba Senegal mabegani jinsi alivyofanya El Hadji Diouf 2002

NA CHRIS ADUNGO

KATI ya mataifa matano yanayowakilisha Afrika kwenye makala ya 22 ya fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar, Senegal ndiyo timu inayopigiwa upatu wa kutamba licha ya kwamba ni itakuwa ikishiriki kipute hicho kwa mara yao ya tatu pekee katika historia.

Mabingwa hao wa Afrika wanaoshikilia nafasi ya 18 kimataifa, wametiwa katika Kundi A pamoja na Uholanzi, Ecuador na wenyeji Qatar. Baada ya kutinga robo-fainali za 2002 wakitegemea huduma za Bouba Diop, Aliou Cisse, Henri Camara na El Hadji Diouf, mara hii wanajivunia maarifa ya kipa Edouard Mendy, beki Kalidou Koulibaly na mvamizi Sadio Mane (nahodha).

Zaidi ya ubunifu na chenga za maudhi, Mane, 30, ana kasi ya ajabu inayomfanya mwepesi wa kuwatoka mabeki kwa urahisi. Alichochewa zaidi kusakata soka kitaaluma baada ya Senegal kufungua kampeni za Kombe la Dunia 2002 kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Ufaransa waliokuwa mabingwa watetezi.

Waliambulia baadaye sare za 1-1 na 3-3 dhidi ya Denmark na Uruguay katika Kundi A na wakadengua Uswidi kwa 2-1 katika hatua ya 16-bora kabla ya Uturuki kuwang’oa kwenye robo-fainali kwa 1-0.

Mane alianza kuchukulia kabumbu kwa uzingativu zaidi baada ya fainali hizo zilizofanyika Japan na Korea Kusini. Aliridhisha katika akademia ya Generation Foot (2009-2011) na akavutia Metz ya Ufaransa iliyojivunia huduma zake hadi 2012.

RB Salzburg ya Austria ilimsajili mwishoni mwa Olimpiki za 2012 zilizofanyika jijini London, Uingereza na umaarufu ukaanza kumwandama mnamo 2014 alipojiunga na Southampton waliomwajibisha hadi 2016.

Kuimarika kwa mchezo wa Mane ulichochea Liverpool kuweka mezani Sh5.5 bilioni mnamo 2016 ili kumshawishi atue ugani Anfield; na akawa mchezaji wa kwanza wa haiba kubwa kusajiliwa na kocha Jurgen Klopp kambini mwa ‘The Reds’.

Tangu wakati huo, alifungia Liverpool mabao 90 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) huku akicheka na nyavu za wapinzani mara 23 kutokana na mashindano yote ya msimu wa 2021-22 ulioshuhudia masogora wa Klopp wakizoa Kombe la FA na Carabao Cup.

Mane, Mohamed Salah na Roberto Firmino waliwezesha Liverpool kutawazwa wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019 kabla ya kunyanyulia kikosi hicho taji la kwanza la EPL baada ya miaka 30 mnamo 2020. Ushirikiano wao, uliokuwa mwiba mkali kwa wapinzani katika EPL na soka ya bara Ulaya, ulizalisha mabao 338 katika kipindi cha misimu mitano kwenye mashindano yote. Mane alipachika wavuni mabao 22 katika EPL mnamo 2018-19 na akaibuka mfungaji bora kwa pamoja na Salah na aliyekuwa mfumaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang.

Nyota huyo atakayevalia jezi za Bayern Munich ya Ujerumani kwa mihula mitatu ijayo akilipwa Sh53 milioni kwa wiki, alibanduka Anfield mwishoni mwa msimu jana baada ya miaka sita iliyomshuhudia akifungia Liverpool mabao 120 kutokana na mechi 269.

Mane aliyekuwa akidumishwa na Liverpool kwa Sh14.8 milioni kwa wiki, aliongoza Senegal kuzamisha Misri kwa penalty 4-2 na kutwaa Kombe la Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza katika historia mnamo Februari 8, 2022 nchini Cameroon. Mwezi uliofuata, Senegal walikomoa Misri kwa penalti 3-1 na kuingia Kombe la Dunia litakalofanyika Qatar kuanzia keshi hadi Disemba 18.

Kufikia sasa, Mane amewajibikia Senegal mara 97 na ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa kikosi hicho kwa mabao 34. Aliambulia nafasi ya pili nyuma ya Mfaransa Karim Benzema kwenye tuzo za Ballon d’Or 2022 baada ya kuibuka Mchezaji Bora wa Afrika.

  • Tags

You can share this post!

Spika wa kaunti amkosoa Koome kuhusu vitisho dhidi ya...

Mitambo na mashine kuboresha kilimo 

T L