• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 12:05 PM
TAHARIRI: Hazina ya Hasla: maoni ya wananchi yapewe uzito

TAHARIRI: Hazina ya Hasla: maoni ya wananchi yapewe uzito

NA MHARIRI

MAAFISA wa serikali wamekuwa wakizunguka kote nchini wakikusanya maoni ya wananchi kuhusu Hazina ya Hustler kabla ya kuzinduliwa rasmi Novemba 30, 2022.

Wananchi wamejitokeza kuelezea wasiwasi wao na kutoa mapendekezo kuhusu jinsi hazina hiyo inaweza kuboreshwa ili kuwahudumia vyema.

Kwa mfano, wakazi wa eneo la Mlima Kenya walitaka riba inayotozwa mkopo wa Hustler iwe asilimia tano badala ya nane iliyowekwa na serikali.

Wanataka mikopo ya chini ya Sh10,000 isitozwe riba.

Hii inatokana na ukweli kwamba wakati wa kampeni muungano wa Kenya Kwanza uliahidi mikopo bila riba kabla ya kubadili kauli baada ya kuingia mamlakani.

Riba ya asilimia 8 inayotozwa mikopo ya Hazina ya Hustler haina tofauti kubwa na riba ambazo zimekuwa zikitolewa mikopo ya simu ambayo imekuwa ikitozwa na kampuni za kibinafsi.

Mkopo wa Mshwari ambao hutolewa na Safaricom, kwa mfano, unatozwa riba ya asilimia 7.5 na ushuru wa asilimia 1.5.
Mtu akichukua mkopo wa Sh500 kutoka kwa Hazina ya Hustler, kwa mfano, atalipa Sh540. Na mwingine kiasi sawa kutoka kwa Mshwari, analipa Sh545.

Hivyo pendekezo kwamba mikopo ya chini ya Sh10,000 isitozwe riba linafaa zaidi ili kutofautisha Hustler Fund na kampuni za kibinafsi.

Aidha, wakulima wanataka kupewa miezi kadhaa kabla ya kuanza kulipia mikopo ya hasla. Kwa mujibu wa wakulima, mazao huchukua miezi mingi kabla ya kukomaa hivyo kuwataka kulipia mikopo kabla ya kuuza mazao yao ni sawa na kuwaadhibu.

Wananchi pia wamekosoa mikopo ya kati ya Sh500 na Sh50,000 inayotolewa kupitia Hazina ya Hustler.

Kiasi hicho cha fedha, kulingana na vijana, hakitoshi kuwakwamua kutoka katika umaskini.

Adhabu iliyowekwa ya Sh10 milioni kwa wanaofuja au kushindwa kulipa mikopo ya Hustler pia imezua hisia kali katika mikutano ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi.

Wakosoaji wanahisi kuwa adhabu hiyo kali huenda ikasababisha idadi kubwa ya walengwa wakaogopa kuchukua mikopo na kukosa kunufaika na Hazina ya Hustler.

Badala ya kuadhibu wanaotumia vibaya mikopo hiyo, serikali ianzishe mpango wa kufunza Wakenya kuhusu namna ya kutumia kiasi kidogo cha fedha kuanzisha biashara.

Lengo kuu la Hazina ya Hustler ni kusaidia mamilioni ya Wakenya wasio na ajira kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha au kuimarisha biashara zao.

Kulingana na manifesto ya Kenya Kwanza, mikopo ya Hazina ya Hustler inalenga kusaidia wahudumu wa bodaboda kuinua biashara zao, kulinda mamilioni ya Wakenya dhidi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwapunja kwa kuwatoza riba ya juu, kuwezesha vijana kunoa vipaji vyao katika usanii na kuwapa walemavu mtaji wa kujiinua kibiashara.

Kuna hatari ya Hazina ya Hustler kukosa kuafikia malengo yake iwapo mapendekezo ya wananchi yatapuuzwa.

  • Tags

You can share this post!

Mitambo na mashine kuboresha kilimo 

JURGEN NAMBEKA: Vijana wajinoe kidijitali msimu wa kuvuna...

T L