• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
MIZANI YA HOJA: Katu usimfanyie ujeuri wala dhihaka mtu yeyote aliyewahi kukutendea wema au kukufaa

MIZANI YA HOJA: Katu usimfanyie ujeuri wala dhihaka mtu yeyote aliyewahi kukutendea wema au kukufaa

NA WALLAH BIN WALLAH

WEMA haununuliwi dukani wala hauchuuzwi sokoni.

Wema hutokana na hulka na utu wa mtu mwenyewe.

Mtu akiamua kuwa mwema atakuwa mwema tu kwa uamuzi wake na hiari yake. Pia akiamua kuwa mwovu atakuwa mkatili kama nyoka.

Lakini ukweli ni kwamba, ni vizuri zaidi kuwa mwema. Ni bora sana kutenda wema maishani. Ni muhimu mno kulipa wema kwa wema. Mtu akikutendea wema usimpuuze wala usisahau wema wake aliokutendea! Kumbuka wema hauozi na mtenda wema hutendea nafsi yake mwenyewe.

Mara nyingi sifa za watu wema hufananishwa na za mitume pamoja na za malaika watakatifu wa mbinguni. Sifa za watu waovu wenye roho chafu aghalabu humithilishwa na sifa za ibilisi.

Kwa hivyo tujitahidi sana tuwe watu wema, tutende mema ili Mwenyezi Mungu atujalie neema na baraka tele kama mitume na malaika.
Watendao mema wapo. Wewe pia ukiamua kuwa mwema utakuwa mwema wa kupigiwa mfano zaidi. Matendo mema hutendwa na kulipwa hapa hapa duniani!

Endapo umewahi kutendewa wema, tafadhali usisahau thamani ya wema maishani.

Daima umkumbuke mtu yeyote aliyewahi kukutendea wema duniani. Usimfanyie ujeuri wala usimwonyeshe kiburi chochote. Usimlipe maovu badala ya kulipa wema kwa wema.

Wapo watu wengi ambao wamewahi kukutendea wema kwa kujua au bila ya wewe kujua umuhimu wa wema wao kwako kama vile wazazi, walimu, waajiri, marafiki, majirani, ndugu na jamaa.

Usiwabeze na kuwapuuza asilani. Uwashukuru. Lipa wema kwa wema.

  • Tags

You can share this post!

Adhabu kali kutolewa kwa mashoga Uganda

Rais wa Tanzania ‘aikejeli’ Kenya kwa...

T L