• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
MIZANI YA HOJA: Omba Mungu sana ili akupe uwezo pamoja na mawazo ya kufikiri uishi vizuri duniani

MIZANI YA HOJA: Omba Mungu sana ili akupe uwezo pamoja na mawazo ya kufikiri uishi vizuri duniani

NA WALLAH BIN WALLAH

KUFIKIRI ni kazi. Kufikiri kunamsaidia mtu kufikiria atakavyoishi, atakavyokula, atakavyovaa na atakavyopata mahitaji yake muhimu duniani!

Kufikiri kunamsaidia mtu kuwaza na kujipangia mikakati ya kukabili shida na matatizo ya ulimwengu!

Kila mtu anajua fika kwamba kuna shida na mazonge mengi tu yanayomkabili kila mwanadamu maishani. Na hakuna njia yoyote ya mkato ya kukabili vikwazo vya maisha duniani bila kuwaza na kuwazua au bila kufikiri na kufikiria kwa makini!

Kosa kubwa ambalo hatufai kuendelea kufanya ni kujaribu kujisahau na kujidanganya kwamba hatuna matatizo ilhali tuna shida na madhila chungu nzima. Tusipokuna vichwa na kufikiria jinsi ya kuyatatua matatizo yetu, tunatarajia nani atakayekuja kufikiri kwa niaba yetu kutusaidia kuyatatua matatizo yetu?

Kila mwaka na kila wakati tunalialia tukilalamika kwamba tuna shida na maisha ni magumu sana! Je, tunatumia vipi muda wetu kufikiria jinsi ya kuyatatua ama kuyapunguza matatizo yetu? Pesa tunazozipata katika kazi zetu au vibarua vyetu, tunazitumia kuyapunguza au tunazitumia kuongeza matatizo yetu maishani?

Kufikiri ni kazi. Tufikirie sana kabla ya kulalamika. Tufikirie zaidi kabla ya kusema na kutoa maneno matupu na ahadi ghushi.

Tufikiri tujue kwamba matatizo yetu ni yetu na watakaoyatatua ni sisi wenyewe. Tufikirie zaidi kuhusu watoto wetu tujue kwamba watakaowasaidia na kuwapangia maisha yao na masomo yao ni sisi wenyewe. Kufikiri ni kazi! Tufikiri.

  • Tags

You can share this post!

Hasara wafanyabiashara wakibomoa vibanda kupisha mradi wa...

Kayole Ladies wapanga jinsi watakavyojitoa mkiani KWPL

T L