• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Mshukiwa mkuu wa bodaboda aliyedhulumu mwanamke anyakwa

Mshukiwa mkuu wa bodaboda aliyedhulumu mwanamke anyakwa

Na SAMMY WAWERU

MSHUKIWA mkuu wa kundi la bodaboda lililodhulumu mwanamke amekamatwa na makachero wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai na Uhalifu (DCI).

Kulingana na DCI, Bw Zachariah Nyaora Obadia alitiwa nguvuni Jumatano eneo la Isebania boda ya Kenya-Tanzania akiwa katika harakati za kutorokea nchi jirani. Aidha, picha ya mshukiwa huyo mkazi wa mtaa wa mabanda wa Mukuru Kaiyaba, jijini Nairobi ilifichuliwa wiki iliyopita.

“Zachariah Nyaora Obadia, mshukiwa mkuu wa tendo la kikatili la unyanyasi wa kijinsia amekamatwa,” DCI ikadokeza, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii. Juma lililopita, idara hiyo ilitoa tangazo la msako mkali dhidi ya Nyaora.

Video iliyofichuka mapema wiki jana na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ilionyesha mwanamke raia wa Zimbabwe akidhulumiwa na wahudumu wa bodaboda.

Inasemakana mwanadada huyo anayesemakana kuwa mwanadiplomasia, alisababisha ajali iliyohusisha mhudumu wa bodaboda na gari lake katika barabara ya Prof. Wangari Maathai, Nairobi.

Kufuatia tukio hilo na ambalo lilizua tumbojoto, Rais Uhuru Kenyatta, aliagiza oparesheni ya kitaifa kwa wahudumu wasiotii sheria za barabara na trafiki. Mamia ya wahudumu na pikipiki zao kutwaliwa, walikamatwa.

Msako huo hata hivyo ulisitishwa mnamo Jumamosi, baadhi ya viongozi wa kisiasa wakikosoa hatua ya serikali kuangazia suala zima. “Nimeongea na Rais Uhuru Kenyatta nikamwambia si wote wabaya. Kama mtu amefanya makosa, ashikwe peke yake.

Hapana shika wale wasio na hatia,” akasema kinara wa ODM, Raila Odinga akizungumza Kisumu kufuatia ziara yake katika kaunti Ijumaa. Bw Raila alikuwa ameandamana na baadhi ya magavana wanaounga mkono azma yake kumrithi Rais Kenyatta, katika uchaguzi mkuu mwaka.

“Sisi kama viongozi tuna uwezo kupata suluhu ya shida katika sekta ya bodaboda. Tupewe wakati,” akasisitiza Gavana wa Kisumu, Prof. Anyang’ Nyong’o. Naye Gavana wa Kitui, Charity Ngilu alisema kuna haja ya wahudumu wa bodaboda kupewa mafunzo yanayohusiana na sheria za barabara na trafiki.

“Hawa watoto ni wetu, si wote wamefanya makosa. Ninaamini Baba (akimaanisha Raila Odinga), utakapochukua hatamu ya uongozi utawapa mafunzo bora,” Bi Ngilu akaelezea, akilalamikia oparesheni ya kuwakamata ilivyofanywa na maafisa wa polisi.

“Si kuwapiga sana, hapo ndio wanapata chakula.” Wakati akitoa amri ya msako, Rais Kenyatta alionya wanasiasa kukoma kuingilia ulainishaji wa sekta ya bodaboda aliyotaja “inahitataji kuwa na nidhamu barabarani”.

Bw Nyaora anatarajiwa kufikishwa mahakamani, kufunguliwa mashtaka. Oparesheni ya kumtia nguvuni iliendeshwa na maafisa wa DCI wenye ujuzi wa masuala ya uhalifu.

Washukiwa wengine 16 wanaendelea kuzuiliwa korokoroni, uchunguzi ukiendelea.

You can share this post!

Chelsea waomba kucheza na Middlesbrough bila mashabiki...

Wakulima wa avokado watumie soko la China kukuza matunda...

T L