• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Wakulima wa avokado watumie soko la China kukuza matunda bora

Wakulima wa avokado watumie soko la China kukuza matunda bora

Na SAMMY WAWERU

FEBRUARI mwaka huu, China ilifungua soko la avokado mbichi zilizokomaa kutoka Kenya.

Hatua hiyo ilitokana na kuendelea kuimarika kwa uhusiano bora wa kibiashara kati ya Kenya na Uchina. Aprili 2019, Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa China, Xi Jinping, walitia saini mkataba wa makubaliano Kenya kuuza mazao yake ya maparachichi nchini humo.

Makubaliano hayo yaliwapa afueni wakulima, japo waliruhusiwa kuuza avokado ambazo zimetolewa maganda na kugandishwa. Mikakati na taratibu hizo za Beijing, zililemea wazalishaji wengi ikizingatiwa kuwa uwekezaji wa mashine ya shughuli hiyo ni bei ghali.

Ni kampuni moja pekee inayouza mazao mabichi ya shambani kimataifa ilimudu, licha ya kuwa na zaidi ya mashirika mengine 100. Tangazo la wakulima kuruhusiwa kuuza avokado mbichi zilizokomaa China, ni afueni.

Maparachichi yakipakiwa katika kampuni ya Kakuzi PLC…Picha/ SAMMY WAWERU

Kutokana na vikwazo ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa, itakuwa busara ikiwa wakulima watajituma kuzalisha mazao yaliyoafikia ubora wa bidhaa – kwa mujibu wa soko la China.

Itakumbukwa kwamba, licha ya Rais Kenyatta na mwenzake Xi Jinping kutia saini mkataba, baadaye Kenya iliwekewa marufuku ya muda. Hata ingawa yaliondolewa, China ililalamikia kusambaziwa maparachichi ambayo hayajakomaa.

Taasisi ya Mazao Mabichi na Mimea (HCD) kwa ushirikiano na ile ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis), ndizo zinajukumika kuhakikisha mazao yanayoingia masoko ya kimataifa yameafikia ubora.

Mashirika hayo, yamekuwa katika mstari wa mbele kuhamasisha wakulima na kampuni zinazowatafutia soko nje ya nchi kuafikia vigezo faafu. “Kenya imepata kibali kuuza avokado mbichi zilizokomaa katika Jamhuri ya Watu wa China,” akatangaza Prof. Theophilus Mutui, Meneja Mkuu Kephis.

Avokado zikipakiwa kwenye makatoni katika kampuni ya Kakuzi PLC…Picha/SAMMY WAWERU

Afisa huyo alisema hatua hiyo iliafikiwa baada ya Kephis na China kutathmini suala la wadudu wanaoshambulia avokado, na jinsi ya kuwakabili. Wazalishaji na wanaouza mazao mabichi ya kilimo masoko ya kimataifa, hawana budi ila kuafikia matakwa yaliyowekwa.

Aidha, yanajumuisha, kuhakikisha mashamba, maghala ya kupakia na vituo vya kutibia maparachichi yao, yamesajiliwa na Kephis. Kulingana na shirika hilo la kiserikali, wakulima watahitajika kuzingatia mbinu faafu kuendeleza kilimo na kukabiliana na kero ya wadudu.

Masoko ya ughaibuni yamekuwa yakilalamikia mazao ya avokado ambayo hayajakomaa, kutoka humu nchini. Mabroka walioteka nyara masoko ya mazao ya kilimo nchini, wametajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo, baadhi wakilaumiwa “kushinikiza wakulima kuvuna maparachichi kabla kukomaa”.

Kulingana na wataalamu, avokado zinazovunwa kabla ya kukomaa ni vigumu kuiva. “Huishia kuharibika na hatimaye kuoza. Mazao ya aina hiyo huharibu soko,” aonya Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya matunda na miti.

Mzee Francis Njoroge, mkulima wa Hass avokado Kaunti ya Murang’a….Picha/SAMMY WAWERU

“Kuna vigezo kadha wa kadha kutambua avokado zilizokomaa. Mosi, matunda kubadili rangi kutoka kijani kibichi na kuwa kijani cheusi. “Mengine, yanakuwa meusi. Vilevile, unapotikisa tunda na kuskia sauti ya mbegu ikicheza, ni ishara kuwa limekomaa,” mdau huyu ashauri.

Maparachichi aina ya Hass yanaendelea kuwa na ushindani mkuu katika masoko ya kimataifa. Yale ya Fuerte, vilevile yanashika kasi. Mzee Francis Njoroge, ni kati ya wakulima wa avokado za Hass, Kenya. Akiwa mkulima wa matunda hayo ya thamani katika Kaunti ya Murang’a, Njoroge anayakuza kwenye nusu ekari.

Kampuni ya Kakuzi PLC, humsaidia kuuza mazao yake katika masoko ya kimataifa. Ni mwanachama wa Kihoto-Kihumbuini Self Help Group, muungano wanaotumia kusambazia kampuni ya Kakuzi kuwatafutia soko.

Kulingana na takwimu za HCD mwaka uliopita, 2021, Kenya iliuza kilo milioni 84.5 ughaibuni kutoka kilo milioni 70.3 mwaka 2020.

: Avokado aina ya Hass zinazoendelea kukua shambani….Picha/SAMMY WAWERU

 

You can share this post!

Mshukiwa mkuu wa bodaboda aliyedhulumu mwanamke anyakwa

Mudavadi: Sera za UDA ziunganishwe na za vyama vingine...

T L