• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Msomaji stadi wa Gazeti la ‘Taifa Leo’ aliyelisoma bila miwani licha ya ukongwe wake azikwa   

Msomaji stadi wa Gazeti la ‘Taifa Leo’ aliyelisoma bila miwani licha ya ukongwe wake azikwa  

NA LAWRENCE ONGARO

MZEE Samuel Gathenya Mugo mwenye umri wa miaka 106 aliyeenzi kusoma Gazeti la Taifa Leo kwa miaka mingi alizikwa kwake Ijumaa, Novemba 17, 2023 katika kijiji cha Muguga, Kaunti ya Kiambu.

Mzee Gathenya, alienzi lugha ya Kiswahili na ndiyo maana alijituma kusoma Taifa Leo kila siku bila kuchelewa, na kusoma bila miwani.

Stadi huyo, kulingana na historia yake alizaliwa mwaka wa 1917 katika kijiji cha Gatunguru, Kaunti ya Murang’a ambapo alifunga pingu za maisha 1946 na mkewe Penninah Wanjiru.

Mzee Gathenya alifariki Novemba 5, 2023 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa wasifu wake (autobiografia), alijaaliwa kupata watoto 12, wana wa kike wakiwa 9, na wanaume 3.

Baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu katika Benki ya Standard mjini Thika, alistaafu mwaka wa 1976.

Baadaye, alizamia katika kilimo huku akiendeleza uraibu wake kusoma gazeti la Gazeti la Taifa Leo.

Ari ya Mzee Gathenya kupenda kusoma Gazeti hili la kipeke la Kiswahili nchini, ilipelekea bintiye Elizabeth wa Njeri Gathenya,  kukienzi Kiswahili.

Wanawe marehemu Mzee Samuel Gathenya wakiomboleza baba yao katika hafla ya mazishi iliyofanyika Ijumaa, Novemba 17, 2023 nyumbani kwake Muguga, Thika. PICHA|LAWRENCE ONGARO

Bi Elizabeth kwa wakati huu ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya upili ya Muhoho, Gatundu Kusini.

Akiomboleza babake, Elizabeth alisema upendo wa Mzee Gathenya kuenzi Kiswahili umemfanya kukuza lugha hii katika Shule ya Muhoho

Shule ya Muhoho imekumbatia lugha ya Kiswahili pakubwa, huku nakala za Taifa Leo zikisambazwa huko kila mara.

Mzee Gathenya aliwapa elimu ya juu wanawe ambapo alizingatia masuala ya masomo zaidi, huku watoto wake saba wakiwa walimu wa shule tofauti nchini.

Jambo lingine kuhusu wanawe Gathenya ni kwamba wanazungumza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha mkubwa.

Wasifu wa Mzee Gathenya ulibaini kwamba alipenda haki, alipenda watu, na kuamini kuwa mali yake yote aliyopata ni kupitia uwezo wa Mwenyezi Mungu.

Bw Francis Mariga Gathenya, mwanawe, ni mjuzi wa lugha ya Kiswahili ambapo alishirikiana na mwandishi wa Taifa Leo, marehemu Hugholin Kimaro kuandika mwongozo wa kitabu cha Kifo Kisimani kitabu kilichotahiniwa kwenye KCSE miaka ya awali.

Kulingana na familia, Mzee Gathenya alianza kusoma gazeti la Taifa Leo 1965.

Bw Mariga alisema uraibu wa Mzee Gathenya kuenzi lugha ya Kiswahili ni kielelezo kwa watu wanaokuza lugha ya Kiswahili.

“Ninatoa wito kwa wasomaji wa Taifa Leo popote walipo waendeleze usomaji wa gazeti hilo ili iwe kama heshima kwa Mzee Gathenya,” alisema Bw Mariga.

Familia hiyo ilipongeza kampuni ya Nation Media, kupitia Gazeti lake la Taifa Leo kwa kuonesha heshima kubwa kwa kumpa Mzee Gathenya heshima ya kuchapisha historia yake magazetini.

 

  • Tags

You can share this post!

Mswada wa kamari kulinda washindi kampuni zisiwapunje

Maskwota 100 washindwa kununua ardhi ya Sh200 milioni

T L