• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
MUME KIGONGO: Gauti: Itakubidi kupunguza pombe na nyama choma

MUME KIGONGO: Gauti: Itakubidi kupunguza pombe na nyama choma

NA LEONARD ONYANGO

NI kawaida kila wikendi kuona makundi ya wanaume wamekusanyika katika maeneo ya burudani wakijiburudisha kwa mvinyo na nyama choma.

Lakini Profesa Omondi Oyoo, mtaalamu wa maradhi ya jongo na mmiliki wa Hospitali ya Nairobi Arthritis Clinic, anaonya kuwa wanaume wanaobugia pombe na kufakamia nyama choma wanajitia katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa gauti (gout).

Kulingana na Prof Oyoo, ugonjwa huu huathiri wanaume zaidi kuliko wanawake.

“Hii ni kwa sababu idadi kubwa ya wanaume hubugia pombe na kula nyama kwa wingi lakini hawafanyi mazoezi,” anasema Prof Oyoo.

Aidha anasema unaathiri viungo vya mwili na husababishwa na kuwepo kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida cha asidi katika damu.

“Pombe husababisha asidi kuongezeka kwenye damu,” anaelezea.

Unapohisi maumivu makali usiku kwenye kidole gumba cha mguu au kwenye magoti au viungo vinginevyo vya mwili, basi hiyo inaweza kuwa dalili ya ugonjwa gauti.

“Mbali na nyama, matumizi ya tembe za aspirini kwa wingi pia kunaweza kufanya damu kuwa na asidi nyingi na kusababisha ugonjwa wa gauti. Mtu hafai kutumia zaidi ya tembe mbili za aspirini kwa siku,” anasema Prof Oyoo.

Ugonjwa wa gauti, hata hivyo, unaweza kutibiwa.

“Ugonjwa huu usipotibiwa kwa muda mrefu unasababisha upele unaojulikana kama ‘tophi’ kumea chini ya ngozi. Aidha, unaweza kudhuru figo,” anasema.

Prof Oyoo anashauri wanaume kufanya mazoezi, kuepuka vyakula vinavyowafanya kuwa wanene kupindukia (overweight) na kunywa maji kwa wingi.

You can share this post!

DKT FLO: Kwa miezi 3 sasa koo yanisumbua

TAHARIRI: Wadau wasikubali propaganda duni zitumike...

T L