• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
MUME KIGONGO: Ole wako ikiwa unapendelea chupi zinazobana na kuoga maji moto!

MUME KIGONGO: Ole wako ikiwa unapendelea chupi zinazobana na kuoga maji moto!

NA LEONARD ONYANGO

WANAUME wanaovalia chupi zilizobana sana na kuoga maji moto kwa muda mrefu wanajitia katika hatari ya kukabiliwa na tatizo la utasa.

Kulingana na wataalamu, chupi (boksa) zilizobana sana na maji moto husababisha joto jingi kupita kiasi katika korodani ambapo mbegu za kiume hutengenezewa.

Mbegu za kiume hutengenezwa katika mazingira ya joto la sentigredi 34 ambalo ni chini ya joto la kawaida la mwili la sentigredi 36. Mbegu huwa dhaifu zinapotengenezewa katika mazingira yenye joto jingi zaidi ya sentigredi 34.

Utafiti uliofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Harvard nchini Amerika, miongoni mwa wanaume 656, ulibaini kuwa asilimia 75 ya waliovalia chupi na suruali za kubana walikuwa na mbegu hafifu.

Watafiti pia walibaini kuwa wanaume waliokuwa wakivalia chupi ambazo hazijabana walikuwa na mbegu za kiume bora na nyingi.

Matokeo ya utafiti mwingine sawa na huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Stanford, Amerika, yalibaini kuwa kulala umevalia chupi zilizobana usiku kunasababisha mbegu za kiume kuharibika.

Wakati huo huo, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha California, ulifichua kuwa kukalia au kuogelea kwenye maji moto kwa muda mrefu kunasababisha mbegu za kiume kuwa hafifu.

Wataalamu wanashauri wanaume kuoga au kuogelea kwenye maji moto kwa muda usiozidi dakika 30 kwa wiki.

Aidha wanasema mambo mengine yanayofifisha mbegu za kiume ni msongo wa mawazo, matumizi ya baadhi ya dawa, dawa za kulevya na kupumua hewa chafu iliyo na kemikali kama vile dawa ya kunyunyizia mimea.

Wanaongeza kuwa baadhi ya tembe kama vile tetracyclines, gentamicin, neomycin, erythromycin na nitrofurantoin zinasababisha mbegu kuwa dhaifu.

Mihadarati kama vile bangi na kokeni inaua mbegu za kiume. Tafiti zinaonyesha kuwa bangi inasababisha mbegu za kiume kuwa mbovu na kubadili umbo.

You can share this post!

Chakula cha msaada chaporwa kutoka kwa lori lililoanguka...

Wahudumu wa boda boda watozwa faini ya Sh7m

T L