• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
MWALIMU WA WIKI: Damaris ni zaidi ya mwalimu bora

MWALIMU WA WIKI: Damaris ni zaidi ya mwalimu bora

NA CHRIS ADUNGO

UALIMU ni kazi inayotaka moyo.

Zaidi ya kuwasilisha somo darasani, mwalimu pia ni mzazi wa wanafunzi wote, rafiki wa karibu, mlezi wa vipaji na mshauri wao kuhusu maisha.

Mwalimu sharti awe na bidii na msukumo wa kutaka kujifunza mambo mapya ili apanue mawanda ya maarifa na ujuzi wake. Apende kusoma vitabu kwa nia ya kujiimarisha na awaulize wajuao zaidi yake ili naye anoe makali yake kitaaluma.

Mwalimu bora anastahili kuwa kielelezo chema na amhimize mwanafunzi kwamba ana uwezo wa kufaulu masomoni. Awe karibu na wanafunzi wake, atambue changamoto wanazozipitia, aelewe kiwango cha mahitaji ya kila mmoja na awaamshie hamu ya kuthamini somo lake.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Damaris Muthusi Kyalo ambaye kwa sasa ni Naibu Mwalimu Mkuu katika shule ya msingi ya Kings International iliyoko mtaa wa Fedha jijini Nairobi.

Damaris anashikilia kuwa mwalimu bora ni mwajibikaji, mbunifu na mwepesi wa kuelekeza wanafunzi kimaadili huku akichangamkia vilivyo masuala yote yanayohusiana na mtaala.

“Mwalimu yeyote aliye na wito wa kufundisha na mapenzi ya dhati kwa taaluma yake, ana jukumu la kuchochea wanafunzi wake kupiga hatua kubwa katika safari ya elimu inayohitaji subira,” anasema.

“Mbali na kuongoza wanafunzi kufikia malengo yao masomoni, mwalimu anapaswa pia kuwa mlezi wa vipaji vya watoto huku akibuni mbinu za ufundishaji zitakazofanya somo lake kuwa la kusisimua na la kueleweka kwa wepesi,” anaelezea.

Damaris alilelewa katika kijiji cha Kitamwiki, Kaunti ya Kitui. Ndiye wa sita kuzaliwa katika familia ya watoto wanane wa Bw John Muthusi na Bi Esther Muia.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kitamwiki kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Mutonguni iliyoko Kitui, kisha akaelekea Nairobi kujifunza ususi, fasheni na masuala ya ulimbwende.

Alisomea uuguzi katika hospitali ya Avenue jijini Nairobi (2000-2002) na akaajiriwa kuwa nesi katika hospitali hiyo hadi mwaka wa 2006.

Kwa kuwa matamanio ya Damaris tangu utotoni yalikuwa kujitosa katika ulingo wa ualimu, alisomea taaluma hiyo katika asasi ya Kindergarten Headmistresses’ Association (KHA), Westlands, Nairobi (2007-2008).

Uamuzi wake huo ulikuwa zao la kuchochewa zaidi na Bw Mureithi aliyemfundisha Kiswahili na somo la Historia katika shule ya upili.

Baada ya kuhitimu, Damaris alifundisha St Christopher’s Group of Schools, Karen mnamo 2009 kabla ya kuhamia Kings International School mwanzoni mwa 2010 kuwa mwalimu wa Kiswahili na somo la jamii. Alipanda cheo kuwa Naibu Mwalimu Mkuu mnamo 2012.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Zetech jijini Nairobi kusomea diploma ya ualimu kati ya 2013 na 2015.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Damaris ni kuwa mhamasishaji wa Kiswahili na kumiliki shule yake binafsi katika siku za usoni.

Amefundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali za maendeleo ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Mama huyu wa watoto wawili – Keith Wambua na Kelsey Mbithe – anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo sasa inatawala walimu wengi ambao hutangamana naye katika warsha za kielimu.

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Ulevi wa Magongo wamtosa mocharini

Mwavumbo bingwa mpya Kwale, Shimba Hills ikilala nusu...

T L