• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Mwavumbo bingwa mpya Kwale, Shimba Hills ikilala nusu fainali

Mwavumbo bingwa mpya Kwale, Shimba Hills ikilala nusu fainali

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

SHULE ya upili ya Mwavumbo walitawazwa mabingwa wapya wa soka ya wavulana kwa shule za upili Kaunti ya Kwale, walipolaza Kinondo Secondary 6-5 mikwaju ya penalti katika fainali iliyochezewa uwanja wa Kinango Secondary, jana Jumapili.

Kocha wa mabingwa hao wapya Alawy Mohamed alikuwa na furaha tele.

“Tumeangusha vigogo hadi kufika fainali. Tunatoa onyo kwa washindani wetu kwamba tumejiandaa kupigania taji la kanda ya Pwani kwa udi na uvumba kushtua hao wanaojifanya miamba,” alisema baada ya ushindi wa kikosi chake.

Kocha wa Kinondo, Hamisi Masusa, alipongeza vijana wake kwa kuwatoa mabingwa watetezi Shima Hills katika kinyang’anyiro cha nusu fainali.

“Wanasoka wangu walitumia nguvu sana dhidi ya Shimba. Lakini sina la kulaumu sababu tumetolewa kwa mipigo ya matuta,” akaeleza Masusa.

Katika mechi za nusu fainali, Shimba Hills ilibanduliwa nje na Kinondo kwa mabao 6-5 ya penalti huku Mwavumbo ikitandika Kaya Tiwi 2-1.

Kwenye fainali ya jana Jumapili, Kinondo ilichukua uongozi kunako dakika ya 33 kupitia guu lake Hamisi Chibulu.

Mwavumbo ikasawazisha kwenye dakika ya 36 mfungajio akiwa Ali Juma.

Katika mipigo ya matuta, Mwavumbo ilipoteza kiki moja wapinzani wakitupa mbili.

Kwenye soka ya wasichana, Mazeras Girls iliibuka mshindi kwa kuilaza Menza Mwenye mabao 2-0.

Mazeras iliitandika Mwangunga Secondary mechi ya nusu fainali nayo Menza Mwenye ikalima Mwereni 1-0.

Matuga Girls ilihifadhi taji la mpira wa magongo ikishinda mechi zake zote na kuwa kileleni mwa jedwali.

Matuga ilizifunga Mackinnon mabao 2-0, Waa Girls 1-0 na Franz Joseph 5-0.

Mvindeni ndio mabingwa wapya wa handiboli baada ya kupepeta Mangawani 14-10 katika fainali.

Kwenye nusu fainali, Mvindeni ililaza Kaya Tiwi 18-13 hali Mangawani ikaishinda Ndavaya 14-12.

Katika handiboli ya wasichana, Kaya Tiwi iliibuka kidedea kwa kuifunga Shimba Hills mabao 7-6 kwenye fainali kali.

Kwenye nusu fainali, Kaya Tiwi na Shimba Hills zilishinda Mwavumbo na Franz Joseph magoli 14-10 na 12-8, mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Damaris ni zaidi ya mwalimu bora

Mabondia wenye uzoefu waduwazwa 24 wakiingia timu ya taifa...

T L