• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
MWALIMU WA WIKI: Makau ni mwalimu stadi na mwandishi

MWALIMU WA WIKI: Makau ni mwalimu stadi na mwandishi

NA CHRIS ADUNGO

AKIJIVUNIA tajriba ya zaidi ya miaka 20 katika taaluma ya ualimu, Bw Silvester Lunyiro Makau anakiri kuwa mtaala wa umilisi (CBC) una nafasi kubwa ya kukuza na kulea vipaji vya wanafunzi kwa kuwa unaegemea zaidi uwezo wao katika fani mahsusi.

“Ni mpango unaoadilisha wanafunzi, kuwajengea msingi wa kukumbatia tamaduni za jamii mbalimbali na kuwachochea kutambua umuhimu wa kuwajibika na kujitegemea,” anaeleza.

Kwa mtazamo wake, mwanafunzi akipata umilisi ufaao, atakuwa wa manufaa katika jamii ya sasa inayoshuhudia mabadiliko ya kasi katika nyanja mbalimbali.

“Kutokana na imani hii, ipo haja kwa mwalimu kukumbatia matumizi ya mbinu zitakazompa mwanafunzi nafasi murua ya kutononoa vipaji vyake na majukwaa mwafaka ya kuchochea ubongo wake kufanya kazi,” anashauri.

Bw Makau kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika shule ya msingi ya Manyole, Nambale, Kaunti ya Busia.

Alizaliwa katika kijiji cha Matawa, Mumias Magharibi, Kaunti ya Kakamega.

Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto sita wa marehemu Bi Josphine Chibete na marehemu Bw Joseph Makau Wayugu aliyewahi kuwa mwalimu na askari wa magereza.

Alianza safari ya elimu katika chekechea ya Matawa mnamo 1986 kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Matawa hadi 1994.

Alisomea katika shule ya seminari ya Mukumu kuanzia 1995 kabla ya kuhamia seminari ya Mama wa Mitume (Mother of Apostles Seminary) mjini Eldoret mwanzoni mwa 1998.

Baada ya kukamilisha KCSE mnamo 1998, alipata kibarua cha kufundisha katika shule ya msingi ya Matawa.

Nafasi hiyo ilimpa jukwaa la kuzima kiu ya ualimu na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Alihudumu huko kwa mwaka mmoja kabla ya kuhamia shule ya msingi ya Mumias D.E.B. alikofundisha Kiswahili, Sayansi, Zaraa na Biashara.

Mnamo 2001, alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Eregi, Kakamega.

Alihitimu kuwa mwalimu wa P1 mnamo 2002 na akaanza kufundisha Kiswahili katika shule ya msingi ya Mumias Central kabla ya kuhamia Mumias Township kisha Imakale, Matungu.

Aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) mnamo 2004 na kutumwa katika shule ya msingi ya Mwitoti, Mumias alikohudumu hadi 2007.

Amewahi pia kufundisha shule ya msingi ya Lureko, Mumias (2012-2014).Kabla ya kuhamia Manyole mnamo Disemba 2019, alikuwa mkufunzi katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Eregi (2016-2019).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini) katika Chuo Kikuu cha Nairobi (2007-2011).

Mnamo 2014, alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya uzamili katika Kiswahili na akafuzu mwaka wa 2022 baada ya kuwasilisha tasnifu “Uchanganuzi wa Uwiano wa Picha na Matini katika Fasihi ya Watoto katika Shule za Msingi za Kaunti ya Kakamega” chini ya uelekezi wa Dkt Pamela Ngugi.

Zaidi ya ualimu, Makau pia ni mshairi shupavu na mwandishi mzoefu wa vitabu na makala ya kitaaluma. Miongoni mwa kazi zake ambazo zimechapishwa ni ‘Lugha na Mtoto’, ‘Lugha ya Pili’, ‘Mfumo wa 8-4-4’, Mtaala wa Umilisi (CBC)’, ‘Nafasi ya Kiswahili katika Ukadiriaji wa Mtaala wa Umilisi Gredi 3’, ‘Jinsi Mtaala wa Umilisi (CBC) Hujenga Stadi za Kiswahili’, ‘Ni Mtihani ama ni Mkadiriaji wa Mtaala wa Umilisi (CBC)?’ na ‘Ufunzaji wa Sauti ‘t’ na ‘d’ kwa kutumia mtindo wa Tusome na CBC’.

Kwa sasa anaandaa kitabu cha hadithi, ‘Njiwa’, kwa wanafunzi wa Gredi 2.

Mnamo 2019, alitunga shairi ‘IOM Japan Hoyee!’ lililokaririwa na wanafunzi wa Kwale Girls ili kuwashukuru wafadhili wa shule hiyo.Kwa pamoja na mkewe, Bi Arnolda Wangatia, wamejaliwa watoto watatu – Emmanuel Murunga, Faith Anyango na Joseph Louise.

Bi Arnolda ni mwalimu wa Sayansi, Kiswahili na Hisabati katika shule ya Nambale Urban, Busia.

  • Tags

You can share this post!

Wanawake wawili taabani kwa kuwaua waume wao

Lionel Messi aongoza PSG kuzamisha Lyon katika Ligi Kuu ya...

T L