• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mahiri na mshairi stadi

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mahiri na mshairi stadi

NA CHRIS ADUNGO

UALIMU ni zaidi ya kazi! Kigezo cha kupimia upevu wa mwalimu ni upana wa uelewa wake wa masuala yanayohusiana na mtaala.

Thamani ya mwalimu huchangiwa na wanafunzi wake. Ukubwa wa thamani hiyo hushinda wingi wa pesa, sifa na vitu vyote vingine vya msimu. Hifadhi ya jina zuri katika fikra za wanafunzi ndiyo malipo bora zaidi ambayo mwalimu hupata.

Mwalimu anapaswa kuwaongoza wanafunzi kwa uangalifu, nidhamu na utaalamu wa hali ya juu. Anastahili kuwa na ufahamu unaozidi wa wanafunzi wake na adhihirishe ubunifu na unyumbufu wake kupitia mbinu za ufundishaji na nyenzo za kuwasilisha somo.

Mwalimu bora anastahili kuwa radhi kujiendeleza kitaaluma na kujifunza mara kwa mara ili kufanya somo lake kuwa la kusisimua na la kueleweka.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Jessicah Rebecca Mkwalafu ambaye sasa ni mwalimu katika shule ya St Patrick’s Makunga mjini Kitale.

“Mwalimu anastahili kuwa nadhifu na mwenye nidhamu. Awe mchangamfu, ajitume ipasavyo na atambue mahitaji ya kila mmojawapo wa wanafunzi wake. Awaelekeze kwa utaratibu unaofaa na awatie moyo hata wasipofaulu kufikia matarajio yake binafsi,” anasisitiza.

Rebecca alizaliwa mnamo 1993 mjini Eldoret, Uasin Gishu akiwa mtoto wa nne kati ya watano katika familia ya Bi Jennifer na Bw John Mkwalafu. Alianza safari ya elimu katika chekechea ya Bondeni, Eldoret kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Nangili kisha shule ya upili ya Moi Girls Nangili, Kaunti ya Kakamega.

Akiwa sekondari, alikutana na Bi Milah Njoroge aliyeshirikiana pakubwa na mwalimu Alfred Alfuma kumwelekeza vilivyo katika uandishi wa insha bora na utunzi wa mashairi.

Baada ya kukamilisha KCSE, alijiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) Bewa la Eldoret kusomea ualimu (Kiswahili na somo la Dini) na akafuzu mnamo 2016.

Mwalimu Jessica Rebecca Mkwalafu anayefundisha St Patrick’s Makunga, Kitale. PICHA | CHRIS ADUNGO

Rebecca aliwahi kufundisha Kiswahili na Sayansi Kimu katika shule ya St Elizabeth Langas, Eldoret mnamo 2014 akiwa bado mwanafunzi wa MKU. Alihamia baadaye katika shule ya Kahoya, Eldoret na akateuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Lugha.

Ilikuwa hadi mwaka wa 2018 alipojiunga na shule ya St Teresa Mukunga, Kaunti ya Kakamega na akaamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi. Mbali na kuwaelekeza wanafunzi wake katika utunzi wa mashairi kwa minajili ya tamasha za kitaifa za muziki na drama, aliwashirikisha pia katika mashindano ya Uandishi wa Insha katika gazeti hili la Taifa Leo.

Wengi wa wanafunzi wake kwa sasa shuleni St Patrick’s Makunga wameanza kutambua utajiri wa vipaji vyao katika utunzi wa kazi bunilizi na huchangamkia sana fursa za kukariri na kughani mashairi katika mashindano ya viwango mbalimbali.

Mapenzi ya kughani mashairi mbele ya hadhira ni fani iliyojikuza ndani ya Rebecca akiwa tineja. Ametunga mashairi mengi kwa matumaini ya kuchapishiwa diwani ambayo anaamini itabadilisha sura ya ujifunzaji na ufundishaji wa Ushairi wa Kiswahili katika shule za upili za ndani na nje ya Kenya.

Kikubwa zaidi kinachomridhisha nafsi ni tija ya kuwaona wengi wa wanafunzi wake wakijitosa katika ulingo wa Kiswahili kwa lengo la kuwa ama walimu, wahariri wa vitabu na wanahabari.

Anaungama kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote hutegemea pakubwa mtazamo wake kwa masomo anayofundishwa na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Uzoefu wake katika ufundishaji wa Kiswahili umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru na Ruto walimana kuhusu shida za Wakenya

Kiganjo Kings inalenga kupanda ngazi msimu huu

T L