• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Uhuru na Ruto walimana kuhusu shida za Wakenya

Uhuru na Ruto walimana kuhusu shida za Wakenya

NA CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto walilaumiana Jumapili kuhusu kilichosababisha tofauti kati yao.

Uhusiano kati ya viongozi hao wawili unaendelea kudorora uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ukikaribia baada ya Rais Kenyatta kumuunga aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuwa mrithi wake.

Akiongea wakati wa sherehe za Leba Dei katika uwanja wa michezo wa Nyayo, rais, bila kumtaja jina, alimtaka Ruto kujiuzulu badala ya kukosoa serikali anayohudumia.

“Ikiwa unahisi kwamba hutaki kunisaidia kutatua matatizo yanayowakabili Wakenya, basi uondoke ili nitafute mtu mwingine wa kunisaidia kazi,” Rais Kenyatta akasema, huku akionekana mwenye hasira.

Kiongozi wa taifa alisema Dkt Ruto ametelekeza majukumu yake na badala yake ameamua kuzunguzuka sehemu mbalimbali nchini kuikosoa serikali.

“Badala ya kuzunguka huku na huku katika masoko, akiandamana na marafiki zao, ukinilaumu kwa kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi, mbona usitoe suluhu kwa tatizo hiyo. Kazi yako ni kudai wewe ni nambari fulani huku ukitoa ahadi ambazo umeshindwa kutimiza wakati huu,” Rais Kenyatta akasema.

“Kwani mimi ni Ukraine? Kwani mimi ni Covid-19?,” akafoka huku akikariri kuwa chimbuko la kupanda kwa gharama ya maisha ni vita nchini Ukraine na janga la Covid-19.

Rais Kenyatta alisema ni baada ya Dkt Ruto kutelekeza majukumu yake serikali ambapo alimsaka ushauri kutoka kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusu mbinu za kutatua changamoto zinazowasibu Wakenya.

“Ndio maana nashukuru huyu mzee kwani hata kama ana matatizo yake alikuja kutusaidia kushughulikia matatizo haya. Yeye sio kama wale wengine wanaotoa matusi na ahadi ambazo hazisaidii chochote,” Rais Kenyatta akasema, bila kutaja majina.

Lakini Dkt Ruto alijiondolea lawama kwa kusema kuwa wale watu ambao Rais Kenyatta aliwapa majukumu yake (Ruto) ndio walifeli.

“Waliporomosha Ajenda Nne za Maendeleo, waliua chama chetu. Wao ni bure kabisa. Boss sijatoroka, ninapatikana kwa urahisi kwa njia ya simu. Inasikitisha kuwa Baraza la Mawaziri halijakutana kwa miaka miwili,” Naibu Rais akasema kupitia ujumbe katika anwani zake za kijamii.

Mwezi Aprili, Dkt Ruto na vinara wenzake katika muungano wa Kenya Kwanza, walidai kuwa Rais Kenyatta na maafisa wakuu katika serikali yake ndio wanafaa kulaumiwa kwa kupanda kwa gharama ya maisha.

“Kupanda kwa gharama ya maisha hakujasababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine wala janga la Covid-19. Lawama inafaa kumwendea Rais Kenyatta na watu wake ambao aliwapa majukumu ya Naibu wake,” akasema kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi Alhamisi wiki jana katika kongamano la kiuchumi kaunti ya Vihiga.

Lakini Jumapili, Rais Kenyatta alisema ingawa Wakenya wanapitia hali ngumu ya maisha kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa nyingine za kimsingi, serikali imeingilia kati ili kuzuia hali kuwa ngumu zaidi.

“Kwa mfano, tulitoa ruzuku ya Sh20 kwa bei ya mafuta. Hii ni maana kuwa bila ruzuku hii bei ya mafuta aina ya petroli ingekuwa Sh177 kwa lita moja. Tumetoa ruzuku sawa na hiyo kwa bei ya dizeli,” Rais Kenyatta akasema.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: ‘Deni’ ametuacha nalo Kibaki kwa...

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mahiri na mshairi stadi

T L