• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu, mwigizaji na mwandishi fasihi

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu, mwigizaji na mwandishi fasihi

Na CHRIS ADUNGO

MWALIMU bora ni rafiki wa wanafunzi anaowafundisha.

Kutokana na urafiki huo, wanafunzi huwa huru kumweleza matatizo yao bila uoga.

Mwalimu aliye karibu na wanafunzi wake hutambua kwa urahisi udhaifu wa kila mmoja wao na hujiweka katika nafasi nzuri ya kuwasaidia na kuwaelekeza ipasavyo.

Mwanafunzi humwamini sana mwalimu ambaye ana ufahamu mpana wa masomo anayofundisha. Hivyo, mwalimu mzuri anastahili kufanya utafiti wa kina katika somo lake na kuchangamkia vilivyo masuala yote yanayohusiana na mtaala.

Awe na uelewa wa stadi mbalimbali za mawasiliano, mwepesi katika kubuni mbinu anuwai za ufundishaji na ajibu maswali ya wanafunzi wake kwa usahihi.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Tabitha Mawia Manzi ambaye sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika eneo la Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Manzi alizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Ngungani, eneo la Mwingi, Kaunti ya Kitui. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bi Rosemary Manzi na Bw Timothy Manzi.

Safari yake ya elimu ilianza katika shule ya msingi ya Ngungani (2001-2006) kabla ya kujiunga na St Francis Kamuwongo Academy, Kitui (2007-2010) kisha shule ya upili ya Kangaru Girls, Kaunti ya Embu (2011-2014). Alisomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya Septemba 2015 na Julai 2019.

Japo alitamani kuwa mwanahabari, Manzi alihiari kusomea ualimu baada ya kuhimizwa na kaka yake, Bw Christopher Kitheka ambaye sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika shule ya upili ya Nyanyaa, Kitui.

Baada ya kuhitimu chuoni, alianza kufundisha katika shule ya Mwihoko, eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kati ya Januari na Aprili 2019.

Mbali na ualimu, Manzi pia ni mwanafasihi chipukizi. Anaamini kuwa sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani yake akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Insha nyingi alizoziandika wakati huo zilimvunia tuzo za haiba na za kutamanisha kutoka kwa walimu wake wa Kiswahili.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango na ngazi mbalimbali na akapata fursa tele za kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Baadhi ya hadithi ambazo Manzi amechangia vitabuni ni ‘Kifo cha Rehema’ katika diwani ‘Kilele cha Mambo na Hadithi Nyingine’ (African Ink Publishers), ‘Msafiri’ katika antholojia ‘Mapenzi ya Pesa na Hadithi Nyingine’ (Williams Publishers Ltd) na ‘Hali Yangu’ katika mkusanyiko ‘Siwezi Tena na Hadithi Nyingine’ (Chania Publishers).

Hadithi zake nyingine ni ‘Wema Hauozi’ katika diwani ‘Mtoto wa Dhahabu’ (Bestar Publishers) na ‘Bamkwe’ katika mkusanyiko ‘Mkaguzi wa Shule na Hadithi Nyingine’ uliochapishwa na Education Distinction.

Ameshiriki pia uhariri wa kazi kadhaa za kibunifu za mwandishi Dominic Maina Oigo pamoja na kitabu cha gredi ya nne kilichoandikwa na Dkt Timothy Arege mnamo 2019 kwa minajili ya Mtaala wa Umilisi (CBC).

Manzi aliwahi kushiriki tamasha nyingi za muziki na drama akiwa mwanafunzi wa shule ya upili na akaongoza Kangaru Girls kutawazwa mabingwa wa kitaifa kati ya 2012 na 2014.

Kwa uelekezi wa Bi Kalange aliyekuwa mwalimu wake shuleni Kangaru Girls, alishiriki pia mashindano ya kutoa hotuba na akawa miongoni mwa wanafunzi walioigiza riwaya ya ‘Kidagaa Kimemwozea’ (Prof Ken Walibora) iliyowahi kutahiniwa katika shule za sekondari nchini Kenya kati ya 2014 na 2017.

You can share this post!

‘Lesso Lessons’ jukwaa mwafaka kuwapa akina mama...

Mwenye baa kuendelea na kifungo kwa kuua mpenziwe

T L