• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
‘Lesso Lessons’ jukwaa mwafaka kuwapa akina mama mafunzo kuhusu lishe bora Kajiado

‘Lesso Lessons’ jukwaa mwafaka kuwapa akina mama mafunzo kuhusu lishe bora Kajiado

Na WINNIE ONYANDO

KAMPUNI ya Roto Tanks ikishirikiana na Ogilvy Africa wiki jana ilizindua mradi wa Lesso Lessons katika Kaunti ya Kajiado kutoa jukwaa la kuwapa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha maelezo kuhusu lishe bora kama njia ya kupambana na utapiamlo katika kaunti hiyo.

Hii ni kutokana na idadi kubwa ya watoto ambao wana utapiamlo katika eneo hilo.

Leso hizo zenye maandishi na michoro maalum zinawapa akina mama maelezo kuhusu vyakula vinavyostahili katika viwango vyote vya ukuaji ili kukuza afia ya watoto.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Roto Tanks, Heril Bangera, alisema kuwa nia yao ni kubadilisha matumizi ya leso na kuifanya kuwa kifaa cha kutolea mafunzo.

“Ni vigumu sana mama anayenyonyesha ama mjamzito akose leso. Hii ndio maana tukaamua kutoa maelezo kuhusu lishe kwenye leso hizo ili kuwasaidia akina mama kupambana na utapiamlo,” akasema Bw Bangera.

Kadhalika, alisema kuwa wanalenga kusambaza leso hizo katika Kaunti zote nchini.

“Tutaunda leso zilizo na maelezo kuhusu lishe kwa lugha zote. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kila mama ana leso iliyo na maelezo kwa lugha yake ya kwanza,” akasema Bw Bangera.

Kampuni hizo zimetoa aina tatu za leso ambazo zina maelezo ya lishe kwa watoto kuanzia mwaka wa kuzaliwa hadi miezi 24.

Kuna leso za rangi ya manjano, kijani kibichi na hata za kijivu.

Kwa upande wake, afisa anayesimamia masuala ya lishe katika kituo cha afya cha Bissil kaunti hiyo, Zaitun Mohamud, alisema kuna haja ya kuwahamasisha akina mama kuhusu umuhimu wa lishe bora.

“Watoto wengi wana utapiamlo na si kwa sababu hakuna chakula ya kutosha nyumbani bali ni kutokana na ukosefu wa uhamasisho na habari za kutosha kuhusu lishe. Baadhi yao wanawaleta watoto wao wakiwa katika hali hatari,” akasema Bi Mohamud.

  • Tags

You can share this post!

Naibu Gavana ashauri vijana kuhusu mafunzo

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu, mwigizaji na mwandishi fasihi

T L