• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Mwanamke Murang’a alivyoshambulia sehemu nyeti za mwanamume aliyetaka kumnyonga

Mwanamke Murang’a alivyoshambulia sehemu nyeti za mwanamume aliyetaka kumnyonga

NA MWANGI MUIRURI

NOVEMBA 4, 2022, Lucy Muthoni, 47, alijipata kwenye njiapanda – alipokumbana na mwanamume aliyekuwa na nia kumuua kwa kumnyonga.

Muthoni, ambaye ni mkazi wa Murang’a anasema mhuni huyo alitaka kumuondoa uhai kwa kutumia kamba.

Mama huyu ni mchuuzi wa matunda katika steji ya Mbombo iliyoko viungani mwa mji wa Maragua.

Anakoishi, ni mwendo wa dakika 20 hivi kutembea na anasema siku ya tukio hakutumia gari la uchukuzi.

“Kama kawaida nikawa nimefunga kazi yangu mwendo wa saa mbili kasorobo na nikaanza mwendo wangu kuelekea nyumbani, nikitumia njia ambayo ilikuwa na vichaka na bila maboma ya watu,” asimulia.

Akiwa ametembea nusu ya kufika kwake, aliona kijana aliyekuwa na nywele za rasta amejitokeza ghafla kutoka kichakani na akiwa amebeba kamba mkononi na ambayo tayari ilikuwa na kitanzi.

“Mshtuko ulionikumba uliniwezesha tu kumuuliza alikuwa nani na nia yake ilikuwa gani. Lakini hakunijibu. Ukali wa macho yake na kila ishara, nikagundua alikuwa anataka kuniweka kitanzi shingoni,” anasema.

Muthoni anasema kwamba alimuomba Mungu wake amnusuru “lakini nikasikia sauti kwa kichwani ikiniagiza nipambane ili Mungu aibariki kazi ya mikono yangu”.

Miereka ikaanza, huku wote wawili wakikabana mabega.

“Niligundua kwamba kijana huyo hakuwa na nguvu za kimwili na nilijaribu kumpokonya kamba aliyokuwa nayo na ambayo katika mabishano yetu alikuwa amejaribu mara kadha kuiweka kwenye shingo langu lakini nikamzima,” anasimulia.

Anaendelea kueleza kwamba jinsi miereka ilivyochacha, ndivyo kijana huyo jambazi aliuma kamba kwa mdomo ili mikono yake miwili imfae katika pambano hilo.

“Nilikuwa nimesikia mahali kwamba ukitaka kumuweza mwanamume katika vita, mkamate nyeti zake na uzivurute ukizipindua ili uchungu umdhoofishe huku akipiga nduru, pia apige magoti akiomba kuachiliwa,” anadokeza.

Na hivyo ndivyo Muthoni alifanya.

“Nilikamata nyeti zake na nikazivuta kwa nguvu zangu zote…Nikazipindua na nikasikia mwili wake umelegea kabisa huku akipiga nduru. Lakini katika harakati hizo za kushabikia ushindi niliokuwa nikipata, nikamwona ameingiza mkono wake wa kulia ndani ya fulana aliyokuwa nayo na kutoa kisu,” Muthoni akumbuka.

Bi Lucy Muthoni akitabasamu wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali katika mtaa wa Mbombo, Maragua, akisimulia alivyopambana na mhalifu aliyetaka kumuua. PICHA|MWANGI MUIRURI

Anasema kwamba alihisi uchungu mkali kichwani mwake, kisha uchungu huo ukahamia mkono wa kushoto nyuma ya bega na mwingine ukamkumba kwenye kifua, upande wa moyo.

“Nilianguka chini nikiwa hoi na nikamwona mvamizi wangu akitoweka gizani. Nilihisi damu yangu ikinuka huku ikitiririka kwa fujo mchangani nikiwa nimelala, uso wangu ukiangalia chini. Nikajua kwamba naiaga dunia,” anasema.

Muthoni anasema alijikaza kisabuni ili angalau afike nyumbani akawaage watoto wake watatu na mumewe, Phillip Kombo ambaye alikuwa ameishi naye katika ndoa kwa miaka 20.

“Nilifika nikiwa hoi na ninakumbuka tu nikiangaliana na mvulana wangu wa kipekee wakati huo akiwa na miaka 13…Nikaskia kwa umbali akipiga nduru na mara miale ya tochi na sauti za watu zikanizingira huku nami nikizimia,” anasema.

Anaelezea kwamba aliamka kutoka kitanda cha Hospitali Kuu ya Maragua baada ya siku tano, na baada ya zingine 10, akapewa ruhusa kurejea nyumbani.

Msimamizi mkuu wa hospitali hiyo Dkt Stephen Ngigi aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba Muthoni alifika katika hospitali hiyo akiwa na asilimia 30 pekee ya uhai wake na ambao ulizama hadi 20 katika siku ya tatu kufuatia kuvuja damu nyingi katika majeraha matatu ya kudungwa kwa kisu.

“Kwanza kisu kilichomdunga upande wa roho kilibakisha wembamba wa nywele kufikia moyo wake…Lakini baada ya kumtoa damu iliyokuwa ikipenyeza kwenye mapafu yake, alirejelewa na asilimia 50 ya uhai na alipopata fahamu zake siku ya tano, ikawa ni asilimia 70 ya matumaini ya kuishi,” anasema.

Dkt Ngigi anasema kwamba baada ya siku 15 akigangwa, Muthoni aliondoka hospitalini akiwa buheri wa afya huku madaktari wakimshukuru Mungu kwa muujiza wa uponyaji.

Hadi leo hii, hakuna mshukiwa ambaye amewahi kutiwa mbaroni licha ya Muthoni kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Maragua.

“Sijawahi kuelewa ni kwa nini kijana huyo alitaka kuniua. Wizi haukuwa nia yake wala kushiriki mahaba. Nilikuwa na simu mbili mfukoni zenye thamani ya Sh20, 000 pamoja na Sh3, 000 ambazo nilikuwa nimeuza matunda. Nia ilikuwa kuniangamiza na kufikia sasa sijawahi kuelewa aliyemtuma,” ansema.

Uvamizi huo ulimtia wasiwasi ambapo licha ya kurejelea kazi yake ya uchuuzi, alikoma kuerejea nyumbani akitembea.

Anasema hutumia huduma za bodaboda.

 mw[email protected]

  • Tags

You can share this post!

GYM za mitaani Nakuru zatajwa kama majukwaa kufunza...

Mambo ni matatu: Gachagua asema yuko tayari ‘kusulubishwa...

T L