• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
MWANAMUME KAMILI: Lau wangalijua utamu wa kuvivalia viatu chaguo lao!

MWANAMUME KAMILI: Lau wangalijua utamu wa kuvivalia viatu chaguo lao!

Na DKT CHARLES OBENE

KUNA rafiki yangu msumbufu aliyenipigia simu akitaka kujua kilicho cha thamani mno kati ya hivi viwili; kiatu kinachositiri mguu ama mguu unaovishwa kiatu?

Nikataka kumwambia azipeleke hurafa kwa watoto wa chekechea. Wajua tena hawa watu wasumbufu walivyojawa kero na kaida za dunia. Kwa kweli alinikumbusha hekima ya kijitoto kilichonitia samli moyoni alipokariri kwamba; afadhali “atupilie mbali pang’anga” lakini katu “hataacha mbwembwe!” Nikatamani kumwambia rakifi yangu hekima ya mtoto yule lakini kwa mara nyingine nikajirudi mwenyewe baada ya kutafakari kwa kina juu ya msemo wa jadi kwamba mja hakatai wito, hukataa aitiwalo.

Mazungumzo baina yetu yalipokita, niling’amua kwamba rafiki yangu hakuwa mwingi wa “pang’anga” kama nilivyodhani. Alikuwa na ujumbe mwafaka unaopasa kutufikia akina sisi tunaotafuta wachumba ama tunaochumbia tu kwa kuwa uchumba na wachumbiao wapo. Kuumeni, kuna watu wanaothamini mno miguu yao kiasi kwamba wanajasirika kuingia kwenye maduka ya jumla wakachagua na kununua majozi ya viatu pasipo kujali bei ama gharama ya viatu. Kwao, miguu ina thamani isiyomithilika.

Kweli, mwanamume kamili huchagua cha thamani mwenyewe akijua thamani yake. Mwanamke kamili hana muda kuchezacheza ama kuchezewachezewa mfano wa “champali!” Sio tukizi waja kuvalia champali kwenye maji ama kuvivuta topeni. Thamani ya champali duni. Vikikatika na vinginevyo viko dukani, tena kwa bei nafuu. Kwa kuwa miguu ya wangwana ina thamani ya juu, watu hawa wanafanya kila jitihada kuhakiki thamani ya kiatu wanachokivalia. Hawa ni wanaume kwa wanawake wanaojitahidi kwanza kuimarisha maisha, kukuza thamani na kuzidisha tija yao. Wanathamini maisha na hali zao kiasi kwamba wanataka kuendeleza hadhi ile kwa kuchagua mchumba anayeweza kufidia bidii ya chudi maradufu. Mwanamume kamili anajua thamani yake na anajua vyema thamani ya kiatu anachotaka kukivaa. Hufanya la tija kutafuta thamani yake. Hujizatiti kuhakikisha kwamba mkewe ama mpenziwe anahitimu, anatimiza malengo yake binafsi. Busara ni mtu kufaana na kiatu chake.

Bila shaka umekwisha kuwaona wanaume kwa wanawake walioekeza muda masomoni wakapevuka akili, wakatimiza malengo ya taaluma na sasa wanavuna matunda ya bidii na ukakamavu wao. Umekwisha kuwaona wanawake waliojibidiisha kitaaluma na kibiashara na sasa ni vigogo tena msingi thabiti kwenye familia zao. Mwanamume kamili anajua maana ya kupiga rangi na kung’arisha kiatu chake. Lipi linaloweza kuzamisha mashua ya wawili wanaofikiria na kutenda kwa umoja na ushirikiano? Tatizo kubwa katika jamii zetu ni kuwepo watu wanaovalia viatu vilivyochakaa kama machaka walikozaliwa. Yaani hawajali hawabali. Kazi yao ni kutafuta kiatu na kukivalia. Kinaya ni kwamba ndio wao hao wanaotafutwa kwa udi na uvumba na majike wa leo. Lau majike hawa wangalijua thamani yao, wasingalichezea maisha yao kufukuzana na magogo ya madume wanaotaka tu kuvalia na kuvivua viatu.

Rafiki yangu aliendelea kunichana na kunichanua kwamba wanawake kwa wanaume wanaofanikiwa kimaisha ni wale wanaojua wanachotaka tena wanaotafuta wanachojua thamani yake. Hiyo ina maana kwamba wanavua kutoka nyanza walizokwisha hakiki wakajua aina ya samaki waliomo. Ole nyinyi mnaoamka kwenye ndoto zenu mkatupa chambo kwenye vijito. Tazama mambo yalivyovurugika kuukeni. Kuna watu wengine wanaonunua viatu tu kwa sababu wanapenda kuona majozi ya viatu mvunguni! Wanapendezwa na kuvutiwa na maumbo sisemi rangi ya viatu. Wakiona viatu vikondevu wanavitaka kwa kishindo. Wakiona vipana vilivyotononoka, wanavitaka kwa mbwembwe. Wakiona virefu wanavidakia kwa mchakacho. Wakiona vifupi vya kukamatia chini ndio hao tayari kwa mchokocho! Ukiwauliza kinachowashawishi kununua majozi baada ya majozi ya viatu, hawana jibu!

Hapo ndipo nilipoanza kunoa ubongo kuyashika ya kushikika barabara. Sio ajabu kuwaona hawa wenye “majozi lukuki ya viatu” wanachakaza ardhini mfano wa kuku wakitafuta vimelea. Mja asiyejua anachokitafuta maishani ni sawia na mwenzake atafutaye asichokijua. Hawa wanaotapatapa gizani kula na mizimwi ndio kwanza balaa beluwa wanaotatiza maisha na kuvuta nyuma gurudumu la maendeleo. Safari ya vipofu wawili hatima yao kidimbwini. Mapenzi ni safari inayohitaji maandalizi kabambe. Tatizo linalotusibu ni kuwepo wapendanao waliogubikwa na joto la mahaba wakasahau umuhimu wa mwanamume kujiweka tayari kabla kupiga mbizi kwenye vidimbwi na kuvua samaki wasioweza kupika wala kula. Lau wangalijua utamu mwanamume na mwanamke kushirikiana na kuvinunua na kuvivalia viatu chaguo lao! Ndivyo wanavyofanya mwanamume kwa mwanamke kamili. Kila mtu anajizatiti kila kukicha kukuza hadhi na thamani ya mwenza. Utu ni kufaana sio kufanana!

[email protected]

You can share this post!

CHOCHEO: Kumchongoa sawa na kuchongea penzi lenu

Hofu ugonjwa wa kutatanisha ukienea Nakuru