• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
MWANAMUME KAMILI: Ole nyinyi mliosikiliza na kusadiki ‘hekima ya kondoo’

MWANAMUME KAMILI: Ole nyinyi mliosikiliza na kusadiki ‘hekima ya kondoo’

Na DKT CHARLES OBENE

NITAANZA kwa hadithi fupi juu ya ‘hekima ya kondoo!’

Asubuhi moja, kondoo alitaka kujua kutoka kwa bwana mmiliki kwa nini anamfunga kamba shingoni ilhali boma lilikuwa limezingirwa na ua na lango kuu lilifungwa kila mara. Isitoshe, kumfunga kamba shingoni kulimnyima uhuru wa kula nyasi zilizokolea umbijani mumo bomani. Alihisi kama kwamba alinyimwa haki kuchagua nyasi za kula kwa wakati uliomfaa kula. Alitaka mmiliki kumwacha huru maana alikuwa amekwisha komaa na anaweza kujifanyia mambo yake mwenyewe kwa wakati uliomfaa yeye. Ndio ‘hekima ya kondoo’.

Baada ya kusikiliza ‘hekima ya kondoo’, mmiliki alikata kauli akamfungua kamba shingoni, akafungua na lango kuu na kumwacha akitamba kwa uhuru huria! Akaulizwa na jirani yake kwa nini ameamua kujitia fedheha namna ile kuamini ‘hekima ya kondoo!’ Mmiliki akajibu kwamba; “uhuru ni uhuru na wanaohitaji uhuru sharti kusikilizwa na kupewa wanacholilia! Mahakama na sheria zipo kwa ajili ya wote wanaokiuka desturi ama wanaovunja sheria!…”

Hadi leo, mmiliki hajapata ondokewa na athari ya uamuzi ule wa kusadiki ‘hekima ya kondoo’. Kwa kufurahia uhuru alioupata, kondoo aliingia hadi sebuleni na chumbani akaharibu mali ya mmiliki. Kwani uhuru aliutaka wa nini? Kondoo alikwisha kataa kula nyasi kila siku kwa kuwa zilimchosha kutafuna. Isitoshe, alivamia mashamba ya majirani akavunja na kuharibu mimea.

Hadi leo kondoo anapigana vita na mmiliki anapojaribu kumfunga kamba. Ameingia ubozi na upumbavu kwa kuwa angali vitani kutaka uhuru wa kufunguliwa kamba na lango kuu. Kondoo ndio kwanza amekwisha tambua maana ya kulilia haki yake. Kondoo angali kwenye maandamano! Mahakama zimejaa kesi za kondoo! Majaji wamechoka kuwaona kondoo kila siku! Sheria hazina makali kuzuia uharibifu wa kondoo! Ole nyinyi mliosikiliza na kusadiki ‘hekima ya kondoo!’

Uhuru na haki

Wanaume kwa wanawake wa leo hawajaacha kulilia haki zao kujieleza na uhuru wa kusema na kutenda jinsi wanavyotaka! Wamepenyeza vipengele tata hadi kwenye Katiba kutaka uhuru wa kusema chochote na kutangamana popote kwa wakati unaowafaa. Mbona kuwadhibiti ilhali ni watu wazima wenye akili timamu, tena wanaojua tosha mbivu na mbichi?

Kondoo ndio hao wanaosimama jukwaani, wakatukana viongozi serikalini, wakasingizia wenzao uhuni na kuwapaka tope! Kondoo ndio hao wanaolipa kondoo wenzao kutatiza mikutano ya wengine ama kuwarushia mawe wapinzani! Kondoo ndio hao wanaoita kondoo wenzao mikutanoni na kuwahimiza kutokubali será za serikali. Kondoo ndio hao wanaochoma vyuo na kuwaua wanafunzi wenzao. Kondoo ndio hao wanaotiririsha machozi ya mamba kutaka haki zao kuheshimiwa ilhali wamekamatwa kwa kiuka haki za wengine! Kondoo ndio hao wanaomiminika kwenye vituo vya polisi kutoa pole kwa wenzao waliokamatwa na kuzuiliwa! Ole nyinyi mliosadiki ‘hekima ya kondoo!’

Sitachoka kuwaelezeni ukweli wa mambo nyie wanaume kwa wanawake majahili wa leo mnaopenda mno kusikika redioni ama kuonekana kwenye runinga. Nani asiyependa sauti na sura yake kutamba ulimwenguni? Nani asiyependa vitendo vyake kujadiliwa na halaiki ya kina yakhe walioketi vijiweni kusubiri na kutafuna ya wenzao walio taabani? Imekuwa kama kazi kila kukicha kusikiliza wanaume kwa wanawake wakitoa ushauri ama maoni kusuhu ndoa za ajabu zinazovunjika na kupatanishwa redioni.

Tazama jinsi uhuru wa kujieleza ulivyotokomeza nchi ya Rwanda miaka ya tisini. Kwa kuwa viongozi waliwafungua kamba shingoni na kuwafungulia lango kuu, wananchi walipeperusha maoni yao redioni walivyotaka, wakapanga mikakati yao peupe na kufanikisha mauaji ya halaiki. Lau kwa ukakamavu na uongozi bora usiosikiliza ‘hekima ya kondoo,’ Rwanda ingalikwisha kitambo! Nchi jirani ya Somalia haijakuwa nchi hadi leo tangu miaka ya tisini. Ilibidi taifa la Kenya kuingilia kati ili kuzuia kuenea kwa ‘hekima ya kondoo!’ Uchumi wa Tanzania unazidi kuwa kwa kasi kuliko uchumi ya taifa la Kenya. Hii ni kwa sababu kuna viongozi wanaojua mwanzo na mwisho wa “hekima ya kondoo!”

Sijui mbona tunazidi laumu serikali hasa wakati huu uchumi unapozidi zorota. Tunatarajia nini katika taifa linalotumia ‘hekima ya kondoo?’ ‘Hekima ya kondoo’ haina nafasi katika taifa linaloazimia kuondoa umasikini, ujinga na upumbavu! Mwanamume na mwanamke kamili sharti kujua vipi kuendesha mambo nyumbani. Kusikiliza ‘hekima ya kondoo’ kisha kufungua kamba na lango kuu ni mwiba wa kujichoma na mtu haambiwi pole.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Kijogoo mtaani, sichoki kuwika’

Liverpool kusajili Florian Neuhaus kuwa kizibo cha...