• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Mzee aliyetumikia ufalme kama dereva asikitika hatakutana na Mfalme Charles

Mzee aliyetumikia ufalme kama dereva asikitika hatakutana na Mfalme Charles

Na WAIKWA MAINA

MZEE ambaye alikuwa akiandamana na Mfalme Charles 111 kila mara alipokuwa akizuru Kaunti ya Nyeri akiwa mdogo, alikuwa na ndoto ya kukutana na mfalme ambaye ziara yake ya siku nne nchini inatamatika leo.

Gathua Kimani, 85 alikuwa dereva wa mbeberu na alikuwa kati ya Waafrika ambao walikuwa wakitangamana na familia ya Mfalme, Malkia Elizabeth, Mfalme Charles na Dadake Anne, ambaye alikuwa mwanamflame.

Mzee Kimani alitangamana na Mfalme na Malkia zaidi ya mara mbili alipokuwa dereva na pia msimamizi wa kitengo cha uchukuzi kwenye Hoteli ya Treetops Nyeri. Kando na kumbukizi zake, kuna picha, vyeti, stakabadhi na jumbe ambazo aliandikiwa ambazo zimeangikwa kwenye nyumba yake.

Kinachoshangaza ni kuwa shaibu huyo anafahamu karibu lugha zote za makabila mbalimbali Kenya. Nyumba yake ni kama makavazi kwa kuwa inaashiria sehemu kubwa ya historia nchini kutokana na jinsi ambavyo, ina stakabadhi na vifaa vingi vya kikoloni.

Nyingi za vifaa na samani alipokezwa na mkoloni kama shukrani kutokana na kazi ambayo alikuwa akifanya. Hasa alikuwa na jukumu la kuwaendesha wageni mashuhuri ambao walikuwa wakitembelea hoteli hiyo na maeneo mengine ya Mlima Kenya.

“Sikupata nafasi ya kumwendesha Mfalme na Malkia japo mara kwa mara nilikuwa kwenye msafara wao. Nilitwikwa jukumu la kuwabeba wageni mashuhuri kutokana na uwezo wangu wa kuzungumza kwa ufasaha,” akasema Mzee Kimani.

“Wakati walikuwa wakizuru Kenya, Mfalme na Malkia walikuwa wakiendeshwa kwenye magari ya serikali. Nilikuwa nahusishwa kwenye mipango ya ziara hiyo. Wakati ambapo nilitangamana na Mfalme, nilimwona kama kiongozi mnyamavu, mpole na mwenye roho nzuri,

“Nilitaka kukutana naye ili nione kama anaweza kunikumbuka. Pia nilitaka kumwasilisha barua kuhusu dhuluma ambayo Wakoloni walitenda familia yangu,” akaongeza.

Alijiunga na usimamizi wa Treetops mnamo 1962 na alikwepo wakati ambapo Mfalme Charles wakati huo akiwa mwanamfalme, alitembelea nchi kati ya 1971-1978 . Alikuwa akiwasimamia madereva kati ya 1971-1987.

“Alikuwa akihudumiwa na maafisa kutoka Huduma kwa Wanyamapori (KWS) huku nasi tukimwendesha alipokuwa akitembelea maeneo mbalimbali. Mara nyingi alikuwa akitembelea msitu wa Aberdare ambayo ni kilomita chache kutoka Treetops” akaongeza dereva huyo.

Mzee Gathua anasema alikuwa anataka kukutana na Mfalme uso kwa macho japo anasikitika kuwa hatakuwa akitembelea Kaunti ya Nyeri.

“Nalaumu kuporomoka kwa Hoteli ya Ark na Treetops kutokana na usimamizi mbaya,” akasema.

Mzee huyo alikuwa kwenye msafara wa Malkia Elizabeth 11 kama dereva mkuu mnamo 1983 wakati ambapo malkia huyo alilala kwenye hoteli ya Treetops. Wakati ambapo mwanamfalme Ann alitembelea Kenya mnamo 1971 na nduguye Charles, ni Mzee Gathua alimwendesha kwa gari kutoka Treetops hadi ikulu ndogo ya Sagana.

  • Tags

You can share this post!

Akothee amuomboleza Ally B, akikumbuka alivyomsaidia kupata...

MCAs wa Nyeri ndio nambari moja katika uchapakazi, utafiti...

T L