• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
NASAHA: Kujitolea kukuza vipaji vya wengine kutakupa fursa ya kujiboresha

NASAHA: Kujitolea kukuza vipaji vya wengine kutakupa fursa ya kujiboresha

Na HENRY MOKUA

WATU wengi husikika wakiguna kila mara Simon Cowell anapomtaka mwimbaji akatize wasilisho lake katika mashindano ya Got Talent.

Umati huwa umeridhishwa na mengi ya mawasilisho anayoyakatiza.

Kumbuka, kufika kwenye jukwaa ambapo Cowell ni mmoja wa waamuzi, mtu huwa ametoa kijasho kweli. Ajabu ni kwamba, miongoni mwa wanaoguna anapolisitisha wasilisho ni waamuzi wenzake. Mbona lakini yeye akose huruma kiasi hicho?

Kimsingi, inaelekea kwamba kila ambapo mtu anaingia jukwaani mara moja hiyo Cowell huwa na matazamio mahususi kumhusu mtu huyo. Anapoanza kuwasili- sha mshindani mwenyewe, mara moja Cowell hugundua mwachano mkubwa baina ya uwezo anaoud- hihirisha mwimbaji na matazamio

aliyomwekea. Sidhani nitakosea kukiri kwamba Cowell ni miongoni mwa watu wachache ulimwenguni ambao wana jicho pevu, moyo mkubwa na mwepesi kwa pamoja. Daima hutaka kilicho bora zaidi ki- jitokeze kwa yeyote anayesimama mbele yake.

Hivi wewe mwalimu, jicho lako ni pevu na lenye upole kiasi gani? Unapomwona mwenzio anafanya vyema hata katika kile mnachoki- wania nyote, wavutiwa, kufurahi na kumpongeza? Mwenzio anapofana katika kufunza somo lake, unakuwa na unyenyekevu kiasi cha kumpongeza na kumhimiza ajitahidi zaidi? Ikiwa mnafunza somo lile lile moja, waweza kuthubutu kumwambia mwenzio kwamba yu bora kuliko wewe ikiwa hiyo ndiyo hali?

Naye mwanafunzi wako anapoibuka kuwa mahiri katika kile unachomwelekeza kwacho, wewe hukiri kwamba amepevuka na kumtaka awe bora zaidi kuliko wewe?

Je, ewe mwanafunzi unao moyo wa kutambua uwezo halisi wa mwenzio? Ukishautambua, unao ujasiri wa kushtakia kwa mwenzio kwamba yeye ni bingwa katika tukio linalohusika. Je, awapo mdogo wako, waweza kujishusha kiasi cha kujifunza kutoka kwake?

Kujidanganya

Kukosa kutambua na kukiri uwezo walio nao wenzako kwa yakini ni kuidanganya nafsi na siku moja kutakusaliti! Jamii yetu ingekuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi endapo tungejifunza kuthaminiana inavyostahiki. Mimi ni mzoefu wa kuwaambia wenzangu kwamba ikiwa kitu ni kizuri, japo ukatae kitasalia kuwa kizuri tu. Kukiri ki kizuri ni kudhihirisha ustaarabu.

Kwa upande mwingine unapodai ni kibaya kutokana na unyonge wako wa nafsi, unasalia na mgogoro baina yako na nafsi yako.

Hii ni fursa nzuri kwako mwal- imu kusema na mwenzio na kum- womba msaada pale ulemewapo. Kumbuka ukiwa mwalimu, haina maana kuwa ni sharti ujue kila kitu kinachohusiana na somo lako. Zaidi ya kufunza, wewe ni mwamuzi – hata suala liwapo geni kwako, unaweza kulichunguza kwa makini na kuamua mwelekeo upi ni sahihi na upi si sahihi kulihusu.

Kwa hivyo, ushikwapo, shikamana! Ninapoandika makala haya, nakumbuka mwaka ambapo baada ya kufunza faslu mahususi ya sarufi, mwanafunzi fulani aliibuka kuwa bora ajabu. Kila akiniletea maswali aliyoyajibu nimtathminie ikiwa ya sahihi, ningemwomba kwanza anieleze jinsi alivyofikiri yeye. Mara karibu zote alizowahi kuja alikuwa sahihi. Mimi ningetoa kauli yangu tu kushadidia: ‘Basi hivyo ndivyo unastahili kujibu’. Leo mwanafunzi huyo yuafunza katika mojawapo ya shule za kimataifa nchini.

Nimemtania majuzi nikimwambia, ‘Nilijua ungefunza katika shule ya kimataifa.’ Haina maana kwamba shule za kimataifa zina hadhi kuliko nyinginezo, la, najaribu kukueleza tu kwamba kuonyesha imani katika mtu, hata awe mdogo wako, kwaweza kuwa kichocheo kikubwa.

Nawe mwanafunzi, acha wivu! Ikiwa mwenzio ni stadi kuliko wewe katika somo fulani, kiri hivyo na mapema. Ama huna habari wivu unaua? Ukishakiri kwa mwenzio alivyo stadi, mwombe kwa unyenyekevu akufae. Nani ajuaye, unaweza kuwa bora hata kuliko yeye wala hatakuchukia kwani ndiwe uliyeugundua uwezo wake halisi!

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Dkt Naomi Musembi

KINA CHA FIKRA: Mafanikio na mazonge tangu tupate madaraka