• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
NASAHA: Matokeo ya KCPE yanampa mzazi na mwana fursa kuwianisha matarajio

NASAHA: Matokeo ya KCPE yanampa mzazi na mwana fursa kuwianisha matarajio

Na HENRY MOKUA

AGHALABU mtu anapowekeza katika shughuli fulani, matarajio yake huwa makuu.

Iwe ni katika shughuli za kilimo, biashara au elimu; aliyetumia raslimali zake katika shughuli mahsusi hutarajia kufaidi.

Utamsikia akitaja matarajio hayo mara kwa mara na kujishawishi kwamba yatatimia. Mtu anapoelekea kumkatiza tamaa labda kutokana na tajriba yake, huondokana naye upesi asije akapanda mbegu za mashaka moyoni mwake. Hatimaye, baadhi huyafikilia matazamio yao huku wengine wakikosa kuyafikilia.

Mitihani si tofauti sana na shughuli nyingine za uwekezaji. Mara si haba, baada ya mwanafunzi kujitahidi kiasi awezacho, hutarajia kufanya vyema. Si kila wakati lakini matokeo yanawiana na matarajio. Katika washikadau watatu wa kimsingi, yaani: mwalimu, mzazi na mwanafunzi, matarajio huweza kutofautiana. Ikifanyika vile, watatu hawa wakashindwa kuwianisha matazamio hayo, huchochea msongo ambao tangu hapo haukosekani. Katika hali hii, wengine hukata au kukatizwa tamaa wasiweze kuwazia ufanisi tena. Hali hii yapaswa kukabiliwa kwa dhati ili isifishe ndoto za mabadiliko chanya.

Katika kipindi hiki baada ya kupokea matokeo ya Mtihani wa Cheti cha Kuhitimu Masomo ya Msingi, kuna haja ya kuwa watulivu na kujaribu kuwianisha matazamio yetu na hali halisi. Kisa na maana, wakati tukipangia shughuli ya masomo na mitihani, huwa kuna changamoto mbalimbali ambazo hatuzitazamii lakini ambazo huchipuka kweli na kutuathiri kwa njia hasi. Changamoto hizi ni pamoja na maradhi, vifo vya wapendwa wetu, uhamisho wa mwalimu aliye kielelezo na mnasihi wa mwanafunzi fulani, utovu wa nidhamu unaochochewa na kuvunja ungo au kubaleghe na nyinginezo. Kama ilivyo kwa mashua baharini, sharti tuachie kiwango fulani cha kusukumwa na mawimbi hivi kwamba matazamio hayawezi kuwiana mia fil mia na matokeo halisi.

Tathmini

Baada ya kupokea matokeo ya mtihani, tathmini jitihada zako wakati wa kujiandaa kwa ajili yayo. Ikiwa kuna moja au mawili ambayo uliyafanya visivyo labda kwa kutojua, jisamehe na uamue hatua ipi itakuwa ya manufaa kwako.

Nawe mzazi, sema na mwanao na kumhimiza kuhusu matokeo yake. Kulalamikia matokeo ambayo hayawezi kubatilishwa hata chembe si wazo la busara. Kumbuka baada ya kupokea matokeo hayo, cha pekee unachostahili kukifanya ni kuyakubali kwanza, hata iwapo hayatakuridhisha. Ukisha, yajadili kwa maelewano na mwanao. Kumzomea katika kipindi hiki ni sawa na kutia msumari moto kwenye kidonda.

Yajadili matokeo yake kwa utulivu muambizane palipokuwa na utelekezi na kutowajibika. Elekezana kwa upole kwani wakati ukidhani uliyatimiza yaliyokujuzu mia kwa mia, umekosea; huenda nawe mzazi ulichangia kufeli kule kwa kiasi fulani. Mkishatambua upungufu uliokuwepo katika maandalizi na wakati wa mtihani, pangia kuukabili upungufu huo katika siku za halafu, wakati mtahiniwa anayehusika akijiunga na ngazi ya sekondari.

Kauli zetu za kipindi hiki zaweza kujenga au kubomoa kabisa. Kwa hivyo, ni muhimu kujituliza kwa muda kabla ya kutoa kauli yako kuhusu matokeo yenyewe. Wapo waliowapa wanao majina ya kutamausha wakajutia kitendo hicho aushini mwao. Wana vilevile wamewahi kuwajibu wazazi wao kwa hasira katika kipindi hiki na kupanda mbegu za uhasama ambao haukuwepo tangu hapo. Kwa hivyo, jadiliana vilivyo na nafsi yako kuhusu utakayo kuyasema ili uwe na hakika kwamba utakapoyatoa yatakuwa ya manufaa.

Hadi sasa sijasema yeyote azembee kazini kwake kwa sababu kutakuwa na mazungumzo ya kuwianisha mambo baadaye, la. Kila mmoja ajitahidi kiasi atakachowezeshwa kwanza, au tuseme, kadri ya uwezo wake kwani kutofanya vile ni msingi wa majuto ambayo kama mjukuu, huja baadaye. Matokeo yatokanayo na jitihada na kujitolea yana utamu; usije ukapitwa na utamu huo.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo

Mwenyekiti wa Juventus akiri kwamba ndoto ya kuwepo kwa...