• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 3:59 PM
Mwenyekiti wa Juventus akiri kwamba ndoto ya kuwepo kwa kipute cha European Super League imezimika

Mwenyekiti wa Juventus akiri kwamba ndoto ya kuwepo kwa kipute cha European Super League imezimika

Na MASHIRIKA

MWENYEKITI wa Juventus, Andrea Agnelli, amesema kwamba mradi wa European Super League (ESL) sasa hautaendelea baada ya kujiondoa kwa vikosi sita kuu vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Agnelli alikuwa miongoni mwa waasisi wakuu wa mpango wa kubuniwa kwa kivumbi cha ESL kilichohusisha vikosi 12 vya Ligi Kuu nchini Uingereza, Uhispania (La Liga) na Italia (Serie A).

Wakuu wa klabu 12 barani Ulaya ambazo Aprili 19, 2021, zilitaka kuasisi European Super League (ESL). Wakuu hawa kutoka juu kushoto hadi chini kulia ni raia wa Real Madrid Florentino Perez, Joan Laporta (FC Barcelona), Enrique Cerezo (Atletico Madrid), Andrea Agnelli (Juventus), Steven Zhang (Inter Milan), Ivan Gazidis (AC Milan), Stan Kroenke (Arsenal), Joel Glazer (Manchester United), John W Henry (Liverpool), Daniel Levy (Tottenham Hotspur), Roman Abramovich (Chelsea), na Ferran Soriano (Manchester City). Picha/ AFP

Hata hivyo, kinara huyo amekiri kwamba kujiondoa kwa washiriki kutoka Uingereza sasa kunamaanisha kuwa haiwezekani kwa kivumbi kipya cha ESL kuendelea.

“Kusema kweli mipango ya kutekelezwa kwa pendekezo la kuanzishwa kwa kipute cha ESL imegonga mwamba. Dalili zote zinaashiria kwamba hatutakuwa na kivumbi hicho kuanzia Agosti 2021 jinsi tulivyotarajia,” akasema Agnelli kwa kusisitiza kwamba kujiondoa kwa Arsenal, Liverpool, Manchester City, Chelsea, Manchester United na Tottenham Hotspur kwenye pambano hilo ni pigo kubwa kwa mradi mzima wa ESL.

Agnelli alijiuzulu wadhifa wake wa mwenyekiti wa Chama cha klabu za bara Ulaya mnamo Aprili 18, 2021 baada ya kutofuatiana na rais wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin aliyeidhinisha mpango wa kupanuliwa kwa ushiriki wa kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kutoka vikosi 32 hadi 36 kuanzia 2024.

Mbali na vikosi sita vikuu vya EPL, miongoni mwa klabu 12 zilizohusika katika hatua ya mwanzo ya kuanzishwa kwa kipute cha ESL ni Atletico Madrid, Barcelona na Real Madrid za Uhispania pamoja na AC Milan na Juventus za Italia. Bayern Munich kutoka Ujerumani walikataa kuhusishwa na mpango huo mnamo Aprili 20, 2021.

Atletico Madrid ya kocha Diego Simeone iliandaa kikao cha dharura mnamo Jumatano ya Aprili 21, 2021 na kufichua mpango wa kujiondoa rasmi kwenye mashindano ya ESL yaliyokuwa yajumuishe jumla ya vikosi 20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

NASAHA: Matokeo ya KCPE yanampa mzazi na mwana fursa...

SAUTI YA MKEREKETWA: Heko tolatola kwa Baraza la Magavana...