• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
NASAHA: Tusaidie katika kutambua na kukuza talanta za wadogo wetu

NASAHA: Tusaidie katika kutambua na kukuza talanta za wadogo wetu

Na HENRY MOKUA

WIKENDI hii nilijaliwa kukutana na mwandishi chipukizi ambaye pia ni mtahiniwa wa Mtihani wa Cheti cha Kuhitimu Masomo ya Msingi (KCPE) mwaka huu.

Nilivutiwa sana kuketi na kumsikiliza kwa makini binti mdogo akitueleza namna alivyoanza safari yake ya kuandika miswada.

Licha ya kwamba hakuwa na mwao kuhusu hatua za kufuata hadi kazi yake ichapishwe, hakufa moyo bali aliendelea tu akiwa na tumaini kwamba siku moja angeyapata maelekezo aliyoyahitaji. Alifurahi sana kuthibitishiwa kwamba talanta ya uandishi anayo na linalohitajika tu ni kuelekezwa hatua kwa hatua hadi stadi za uandishi zikolee akilini mwake.

Inasikitisha kwamba licha ya talanta hii inayofaa kufurahiwa hata na adui zake, wengi wa jamaa zake wameshakerwa naye. Iweje wanahisi kwamba binti mdogo anapoteza muda wake wa kusoma ili aupasi mtihani wake na kuja kufanya kazi ya maana katika siku za halafu! Mbona wazazi na waangalizi tumechanganyikiwa sana hivi? Unaipuuzaje talanta ya wazi kama hii wakati waja wengine wanajitahidi kuzigundua talanta zao au hata za wanao wasione kitu! Roho kama huyu anafaa kulaaniwa kwa kinywa kipana kwani hivi ndivyo ndoto za watoto wengi zinavyokandamizwa na hatimaye kufishwa!

Ama kwako wewe mwanafunzi uliyeigundua talanta yako, zichukulie changamoto kama kichocheo cha kukitia makali kipaji chako. Niliwahi kumwambia binti wa kisa na mkasa kwamba kazi ya uandishi hasa hunawiri hali inapokuwa hiyo ya kurushwarushwa na mawimbi. Sisemi kwamba changamoto zibuniwe hata ambapo hazipo, badala yake ninahimiza kwamba zikija, wakati zikiendelea kutafutiwa suluhisho, unakuwa na upenyu wa kuyaelewa mambo ambayo wanajamii wengine huyapitia.

Kwa msingi huu unaweza kufanya vyema zaidi katika kuikuza talanta yako. Nililithibitisha hili nilipoangalia baadhi ya anwani za kazi za mwandishi chipukizi ninayemrejelea. Anwani hizo zinadhihirisha ubunifu mkubwa na zinao mnato wa aina yake. Nauhusisha ubunifu huu na mnato wa anwani zenyewe na changamoto anazozipitia kwa sasa.

Ukandamizaji

Ukiikandamiza talanta ya mwanao kwa sababu umeijua, utakuwa unampa sababu ya kutafuta mbadala wa kuikuza mbali na wewe. Hatari iliyopo ni kwamba hutamjua hata mwelekezi wake wala mengine atakayomfunza. Ni jambo la busara daima kukiri kwamba umekitambua kipaji cha mwanao na kumpa mwongozo stahiki wa kuufuata ili kuikuza talanta yake ipasavyo.

Wapo wale ambao wamewahi kuninongónezea kwamba walizitalii talanta zao wakati wa likizo ndefu bila wazazi wao kungámua hata chembe kwamba walikuwa wanafanya vile. Wapo waliolipwa hela za haja kutokana na vipaji hivyo vyao nami kwa kupenda kuzikuza talanta nawafurahikia ajabu. Lililosalia sasa ni kuongoza shughuli ya mzazi kuyajua na kuyanasihi makundi yote mawili kuufikilia mwafaka ili yeyote baina yao asisalie akizishuku hatua na matokeo ya hatua za mwenziwe kati ya mwana na mzazi.

Jambo la kutia moyo ni kuwa Mungu ana namna ya kumwibua mkombozi hata pasipotarajiwa. Yupo shangazi ya binti ninayemsimulia aliyeifanya kama mzigo wake shughuli nzima ya kumtambulisha kwa watu wanaoweza kuwa wa msaada katika kukikuza kipaji hiki adhimu. Nilimfurahikia sana na kumtakia baraka tele kwa kuchukua hatua ya kishujaa kumwajibikia mwana huyu kama ambavyo wazazi wake wangefanya.

Ewe mwanafunzi uliyegundua talanta yoyote iwayo muradi inawiana na imani, mila na desturi zenu na maadili ya jamii kwa jumla, chukua hatua kumwarifu yeyote utakayemwaminia taarifa hii kwamba unacho kipaji hicho. Hivi ndivyo kipaji chako kitapata kuona mwanga wa jua na kuanza kukua.

Nawe uliye karibu na mwanafunzi kama huyu, mfae kwa kumhimiza na kushauriana na wengine wanaoweza kumfaa. Zaidi ya hivyo, mtambulishe kwa wengine wanaoweza kuwa wa msaada kwake na baraka zisizokadirika zitakuandama.

You can share this post!

NGILA: Nchi za Afrika zikumbatie teknolojia kama Kenya

Kamworor na Obiri watiwa kwenye orodha ya wanariadha...