• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
NGILA: Nchi za Afrika zikumbatie teknolojia kama Kenya

NGILA: Nchi za Afrika zikumbatie teknolojia kama Kenya

Na FAUSTINE NGILA

KATIKA Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), abiria kutoka mataifa mbalimbali wanatoka kwa ndege zao na kufululiza moja kwa moja hadi eneo la kupimia virusi vya corona.

Kamera za kiotomatiki zenye uwezo wa kupima joto mwilini kwa watu kama hamsini hivi kwa mpigo, zimewekwa kwenye kuta, huku matokeo yakionyeshwa kwenye skrini kubwa.

Hii ni teknolojia mpya iliyobuniwa kupitia ushirikiano wa Umoja wa Afrika (AU), shirika la PanaBIOS na kampuni ya humu nchini ya Kodchain inayowezesha serikali kuthibitisha uhalali wa vyeti vya corona kupitia jukwaa la mtandaoni.

Naweza kusema kuwa Kenya imekuwa mstari wa mbele katika matumizi ya teknolojia za kiafya, lakini kwa kuwa taifa la kwanza barani kutumia ubunifu huo ni ishara kuwa mataifa ya kigeni yanatuaminia kwa mapenzi yetu ya kutumia teknolojia kusaka suluhu za changamoto zetu.

Antonia Filmer, mfanyabiashara kutoka Uingereza alisema majuzi kuwa akilinganisha na London, Nairobi imeweka mfano mwema kwa mataifa ya Ulaya ambapo itakuchukua zaidi ya saa nzima kukaguliwa kwenye uwanja wa ndege ikilinganishwa na dakika 15 pale JKIA.

Wiki iliyopita, Kenya ilipokea roboti tatu zenye uwezo wa kupima watu 100 joto mwilini kwa dakika moja, huku zikipulizia dawa mazingira ya umma. Ishara nyingine ya jinsi mataifa yaliyoendelea yanatambua Kenya.

Hivyo, ni heko kwa Wizara ya Afya, kukubalia matumizi ya ubunifu wa AU, hasa ikizingatiwa Kenya inahitaji kujinyanyua kiuchumi kutokana na pigo la corona ambalo limesambaratisha biashara tangu Machi mwaka uliopita.

Ubunifu huo tayari unawavutia wawekezaji kutoka mataifa mengine, na kuboresha brandi ya Kenya kimataifa hali ambayo itachangia pakubwa katika ukuaji wa biashara humu nchini ikilinganishwa na taifa lingine lolote barani.

Kwa kutekeleza mpango huo, pia JKIA inapunguza idadi ya maambukizi mapya yanayoingia humu nchini na yale yanayopelekwa katika mataifa mengine, kwani teknolojia hiyo ina uwezo wa kutambua walio na joto kupita kiasi.

Pia, ni suluhu tosha kwa matapeli wa kimataifa wanaotumia vyeti feki vya corona kuingia humu nchini. Inasaidia kukamata watu kama hao kwa kuvunja sheria za Kenya.

Isitoshe, safari za ndege humu nchini zitaongezeka, watalii wakijihisi salama kiafya na kutopotezewa muda JKIA wakisuburi maafisa wa uhamiaji kuwakagua.

Hii ni fursa ya mataifa mengine ya Afrika kujifunza kutokana na Kenya, na kuanza kutumia teknolojia hiyo ambayo inatolewa bila malipo na kupiga jeki juhudi za kuinua Afrika kwa jumla kutoka lindi la kudorora kwa uchumi.

Haina faida taifa moja pekee kutumia teknolojia hii. Inapaswa kuwa ni mataifa yote 54, hata yale yasiyo na viwanja vya ndege yanafaa kutumia ubunifu huu kwenye mipaka ili kuzuia maambukizi na kuleta imani katika shughuli za biashara baina ya mataifa.

Iweje umetumia dakika 15 JKIA kuabiri ndege ila unasubiri kwa saa mbili jijini Johanesburg ukikaguliwa? Hiyo inakuchelewesha na hata kuharibu mipango yako ya biashara Afrika Kusini.

Lakini mataifa mengine yote 53 yakikumbatia teknolojia hii, Afrika itaweza kuinuka pamoja, kushikana mkono na kufaidika pakuu kiuchumi.

You can share this post!

Chipu kutetea Kombe la Afrika mwezi Machi, ratiba ya...

NASAHA: Tusaidie katika kutambua na kukuza talanta za...