• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
NGUVU ZA HOJA: Chuo Kikuu cha Baraton ni mfano wa kuigwa na asasi za elimu ya juu

NGUVU ZA HOJA: Chuo Kikuu cha Baraton ni mfano wa kuigwa na asasi za elimu ya juu

NA PROF CLARA MOMANYI

KATIKA makala yangu ya tarehe 1/9/2022 niliweka bayana umuhimu wa Tume ya Mackay katika kusimika matumizi ya Kiswahili nchini.

Ijapokuwa pendekezo la Tume hiyo la kufundisha Kiswahili kama somo la lazima hasa katika Chuo Kikuu cha Moi halikufuatiliwa, Chuo Kikuu cha Baraton kiliona umuhimu huo.

Chuo hiki hutoa mafunzo ya Kiswahili ambayo ni ya lazima kwa wanafunzi nchini na kwingineko janibu za Afrika Mashariki.

Mojawapo ya sera za chuo hiki ni kuwa, Kiswahili kifundishwe kama somo la lazima kwa wanafunzi wote wanaosomea taaluma mbalimbali hususan wale wanaotoka maeneo ya mashariki mwa Afrika.

Isitoshe, wanafunzi wanaotoka nje ya Afrika Mashariki pia wanaruhusiwa kusoma Kiswahili au Kifaransa ili kutosheleza mahitaji ya lugha kama sehemu ya masomo yao.

Chuo cha Baraton kiliamua kutoa mafunzo ya lazima katika Kiswahili kutokana na taaluma mbalimbali zinazofunzwa chuoni humo kama vile utabibu, ualimu, sayansi na masomo ya sanaa miongoni mwa taaluma nyingine.

Bila shaka, Chuo hiki kinaelewa kwamba wahitimu wanahitaji kuwa na umilisi wa Kiswahili hususan pale wanapoenda kutekeleza majukumu yao nyanjani.

Hii ni hatua muhimu inayohitaji kuigwa na vyuo vyote nchini ili kuondoa vikwazo vya kimawasiliano hasa wakati wa kutoa huduma kwa umma.

Miongoni mwa wahadhiri walioweka msingi madhubuti wa kuandaa mitaala ya ufundishaji wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Baraton ni pamoja na Prof Miriam Mwita na Prof Samuel Obuchi.

Kutokana na mfano bora uliowekwa na chuo hiki, litakuwa jambo stahilifu kwa wizara na taasisi zinazohusika na uundaji wa sera za elimu ya juu kutathmini uwezekano wa Kiswahili kufundishwa kama somo la lazima katika vyuo na taasisi zote za elimu nchini.

Kiswahili ni lugha ambayo haiwezi kupuuzwa katika elimu ya juu kutokana na nafasi yake ulimwenguni.

  • Tags

You can share this post!

Haaland atambisha Man-City dhidi ya Borussia Dortmund...

PSG watoka nyuma na kuzamisha chombo cha Maccabi Haifa...

T L