• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:24 PM
NGUVU ZA HOJA: Kiswahili ni mhimili mkuu wa kuhifadhi fasihi yetu ya jadi

NGUVU ZA HOJA: Kiswahili ni mhimili mkuu wa kuhifadhi fasihi yetu ya jadi

NA PROF CLARA MOMANYI

KISWAHILI ni lugha ya Kiafrika ambayo inaweza kuwa mhimili mkuu wa kuhifadhi fasihi jadi ya jamii zetu.

Katika kipindi cha ukoloni na hata baadaye, kulikuwa na ukengeushi mwingi miongoni mwa Waafrika hususan katika kutumia lugha zao asilia.

Baadhi yetu tuliathiriwa na mielekeo ya kimagharibi, tukakengeuka kwa kudhani kuwa chochote kilichoasisiwa na Mwafrika katu hakiwezi kusimama kama hakina ‘uzungu’ ndanimwe.

Tulikengeuka kimawazo tukaanza kudharau vyakula vyetu, mavazi hata majina yetu!Lakini tokea mwaka wa 1934, aina fulani ya vuguvugu ambalo tunaweza kuliita Uafrika’ (Negritude) liliasisiwa na Waafrika mashujaa kama vile Leopold Sengor wa Senegal, Kenneth Kaunda wa Zambia, mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania miongoni mwa wengine.

Mbali na kwamba wazalendo hawa walipendekeza matumizi ya lugha moja ya kiasili kama kiungo muhimu cha kueneza umoja wa jamii zetu, mawazo yao yalichochea baadhi ya wanafasihi na wasomi wa Kiafrika kuanza kujitathmini upya. Walianza kusaili uasili na falsafa ya Mwafrika.

Katika miaka ya 1970, mwamko mpya wa kuhifadhi maadili na falsafa ya Mwafrika ulitiwa mbolea na kuchipuza. Mwafrika akaanza kuthamini vyakula, mavazi na majina yake.

Ijapokuwa Kiswahili kina historia ndefu ya uandishi wa fasihi, karne iliyopita ilishuhudia makuzi makubwa ya uandishi wa fasihi ya Kiswahili Afrika Mashariki hasa kwenye miaka ya 1970 kutokana na mwamko huo wa Kiafrika.

Hivyo basi, ni jambo stahilifu kutumia Kiswahili kuhifadhi masimulizi jadi ya jamii zetu.

Tufahamu kwamba tuna machimbo mengi ya simulizi jadi ambayo yanaweza kuhifadhiwa kupitia kwa uandishi wa fasihi.

Kutokana na matumizi mapana ya Kiswahili, tunaweza kuhifadhi na kusambaza fasihi zetu asilia ambazo zimepuuzwa na ziko katika hatari ya kusahaulika.

  • Tags

You can share this post!

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya Upili ya...

LISHE: Chagua chakula chenye manufaa kwa mtoto

T L