• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
NGUVU ZA HOJA: Tuwafanye raia wa kigeni nchini kuwa mabalozi wema wa lugha ya Kiswahili

NGUVU ZA HOJA: Tuwafanye raia wa kigeni nchini kuwa mabalozi wema wa lugha ya Kiswahili

NA PROF IRIBE MWANGI

JUMA lililopita Chuo Kikuu cha Nairobi kiliadhimisha Siku ya Wanafunzi wa Kigeni. Chuo kina wanafunzi wa kigeni wapatao 2,000.

Ilikuwa furaha kwao kujumuika na Wakenya. Nilifurahia zaidi ngoma za kiasili kutoka Burundi, Somalia na Sudan Kusini.

Mawasilisho yakiendelea, nilipata akili yangu ikitalii nchi za kigeni nilizowahi kutembelea na tajriba zangu kama mgeni.

Tatu ya safari hizo ziliganda katika akili yangu, mbili katika nchi ya Uchina mnamo 2010 na 2012 na nyingine Ujerumani mnamo 2016. Nilikumbuka tulivyotaabika katika duka la kuuza dawa jijini Chang Chun tukijaribu kueleza tatizo letu kwa Kiingereza kwa wauzaji walioelewa Kichina pekee.

Nilizinduka na kumpata John Orindi, Mkurugenzi wa Mawasiliano chuoni, akieleza faida za kuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Kati ya nyingi alieleza ile ya kujifunza lugha tofauti kama vile “Kichina, Kikorea, Kireno, Kifaransa, Kijerumani na Kiswahili bila malipo.”

Japo sikufurahia mpangilio wake (nilitaka lugha ya Kiswahili iwe mwanzo kwa kuwa ndiyo asilia), nilikubaliana na mawazo yake.

Lugha ni chombo muhimu sana kwa mgeni yeyote. Humwezesha kuwasiliana na hivyo kukidhi mahitaji yake ya kimsingi.

Nchini Kenya, Kiswahili ndiyo lugha ya msingi imwezeshayo mwanafunzi wa kigeni kukidhi mahitaji yake ndani na nje ya chuo.

Wanaposafiri kurejea kwao, kama alivyoeleza Mtiva wa Wanafunzi Joshua Kinyua, hawa huwa mabalozi wa kueneza lugha na utamaduni.

Matatizo ya kimawasiliano niliyokumbana nayo Uchina na Ujerumani ndiyo yaliyofanya nizikumbuke nchi hizo siku hiyo. Ni muhimu kujifunza lugha nyingi, hasa za wenyeji.

  • Tags

You can share this post!

Murkomen ataja hatua zinazolenga kupunguza vifo Thika...

NGUVU ZA HOJA: Tuhifadhi kiteknolojia utajiri wa fasihi...

T L