• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
NGUVU ZA HOJA: Tuhifadhi kiteknolojia utajiri wa fasihi yetu ili tufae vizazi vijavyo

NGUVU ZA HOJA: Tuhifadhi kiteknolojia utajiri wa fasihi yetu ili tufae vizazi vijavyo

NA PROF CLARA MOMANYI

FASIHI ni njia moja ya kuendeleza utamaduni wa jamii ambao pia ni ujumla wa maisha ya jamii hiyo.

Kupitia kwa fasihi, jamii huweza kuhifadhi na kuendeleza mila, desturi, miiko, itikadi au hata falsafa yake.

Fasihi hutumiwa kutoa mafunzo mema, maarifa na hekima miongoni mwa wanajamii.

Fasihi ambayo pia hufunzwa shuleni, inaweza kutumiwa kujenga hulka nzuri miongoni mwa wanafunzi.

Kenya ni nchi iliyobarikiwa kuwa na jamii nyingi, na kwa hivyo kuna dafina kubwa ya fasihi iliyosheheni katika jamii hizo.

Je, fasihi hii hutumiwa kikamilifu kuwaelekeza, kuwafunza, kuwakosoa au kuwaelimisha watoto wetu kama ilivyokuwa zamani? Jibu ni la, hasha. Sababu za sisi kutoweza kuendeleza mafunzo ya hekima kupitia kwa fasihi zetu ni nyingi, zikiwemo mabadiliko katika mifumo ya kutoa mafunzo kwa watoto na mienendo mipya ya maisha miongoni mwa jamii zetu.

Katika miongo kadha iliyopita, tumeshuhudia masimulizi jadi ya jamii zetu yakipuuzwa huku fasihi za kigeni na njia mpya za kuzisambaza zikichukua nafasi kubwa miongoni mwa watoto na vijana nchini.

Kukumbatia maadili ya kigeni na kudharau mafundisho na maadili katika fasihi zetu ni sawa na kutupa tamaduni na asili zetu huku tukiupisha ugeni utawale fikra, mielekeo na maadili yetu.

Simulizi kama vile visasili au semi kama vile methali, mafumbo na vitendawili huwa na mafundisho mema yaliyosheheni busara, hekima na maarifa kwa jamii iliyoziunda.

Nina hakika kwamba kuna utajiri mkubwa wa simulizi za jamii zetu ambao nahofia huenda ukapotea kutokana na kutotumiwa au hata kutohifadhiwa ipasavyo.

Zipo fasihi za baadhi ya jamii zetu zilizohifadhiwa kimaandishi au katika kanda za video lakini idadi kubwa ya jamii zetu haijawa na njia bora za kuhifadhia dafina hii muhimu.

Kutokana na hili basi, ipo haja kwa watafiti na wanafasihi kuhifadhi fasihi mbalimbali za jamii zetu kupitia kwa njia za kiteknolojia ili ziweze kufaa vizazi vijavyo.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Tuwafanye raia wa kigeni nchini kuwa...

Mung’aro aunga azma ya Kingi kuwa rais 2032

T L