• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:31 PM
NGUVU ZA HOJA: Ulimwengu wa Kiswahili waenzi mwandishi mashuhuri wa Fasihi na Isimu Said Ahmed Mohamed

NGUVU ZA HOJA: Ulimwengu wa Kiswahili waenzi mwandishi mashuhuri wa Fasihi na Isimu Said Ahmed Mohamed

NA PROF IRIBE MWANGI

MARA ya kwanza “nilipokutana” na Prof Said Ahmed Mohamed ni wakati mwalimu Alex Ngure alipotuongoza kuchambua mashairi ya diwani Kina cha Maisha aliyoyaandika Said.

Niliyapenda mashairi hayo na hadi leo nakumbuka baadhi yayo kikamilifu.

Diwani hiyo ilinishajiisha kuupenda ushairi na hatima yake ni diwani niliyoihariri na K.W. Wamalwa, Miali ya Ushairi.

Baadaye, nilipojiunga na Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Nairobi nikiwa mwanafunzi nilikutana na Said ana kwa ana.

Sikuamini kwamba mwandishi niliyemsoma na ambaye kufikia wakati huo Prof Kineene wa Mutiso alikuwa ametupa orodha ndefu yenye vitabu alivyoviandika, ndiye aliyekuwa akisimama mbele yangu akinitanguliza kwa somo jipya: Isimu.

Kamwe sitawahi kumsahau akitufunza hadi kutokwa na jasho huku akituelekeza kwenye mawazo ya Ferdinand de Saussure na Noam Chomsky.

Prof Said Ahmed Mohamed. PICHA | MAKTABA

Huyu ndiye mwalimu, mwandishi (wa zaidi ya vitabu 30), mwanaisimu, mwanafasihi, muundaji maneno na msambazaji mkubwa wa Kiswahili ambaye aliuleta pamoja ulimwengu wa Kiswahili Jumapili tarehe 30 Aprili.

Katika kongandao lililoandaliwa na Nadj Media (Najma Khamisi) kwa ushirikiano na CHAWAKI (kikiwakilishwa na Hezekiel Gikambi, nami), wazungumzaji kutoka Pemba, Kenya, Ujapani, Ujeremani, Uingereza, Uchina, Tanzania, Uganda na takriban kila pembe ya ulimwengu, walimuenzi Said angali hai.

Japo anaugua, habari tulizozipokea kutoka kwa familia ni kwamba alifuatilia mazungumzo hadi mwisho. Alifurahi sana!

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Matunda ya kwanza kabisa ya mtaala mpya wa...

VALENTINE OBARA: Wadau wa utalii Pwani wawe wabunifu...

T L