• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
VALENTINE OBARA: Wadau wa utalii Pwani wawe wabunifu kujivumisha kote

VALENTINE OBARA: Wadau wa utalii Pwani wawe wabunifu kujivumisha kote

NA VALENTINE OBARA

KATIKA enzi hizi za mawasiliano kidijitali, kuna mambo mengi ambayo mashirika yanaweza kutimiza mitandaoni kwa juhudi za kujiinua kibiashara.

Mara nyingi watumizi wa mitandao hasa ya kijamii wameshuhudia jinsi mashirika mbalimbali huwa hayapotezi muda wowote yanapoona mwanya wa kutumia kujitangaza.

Hii huonekana kupitia kwa matangazo ya ucheshi, video, matukio ya kipekee na kadhalika.

Hapa, matangazo husukwa kwa mbinu inayovutia wengi ili watu wanapojifurahisha, wanapata pia kujua mengi kuhusu shirika husika.

Narejelea haya kwa vile, hivi majuzi, sekta ya utalii hasa eneo la Pwani ilikosa nafasi nzuri ya kujitangaza kwa mapana kimataifa.

Wiki iliyopita, Wakenya waliamkia habari kuwa gwiji wa soka ulimwenguni, Samuel Eto’o, alikuwa amezuru maeneo ya Malindi pamoja na familia yake.

Ziara hiyo haingelifahamika na wengi endapo mwanasoka huyo mstaafu aliyechezea timu ya kitaifa ya Cameroon hangetangaza safari yake katika mitandao ya kijamii.

Eto’o ambaye amewahi pia kuchezea timu za kandanda za Barcelona, Chelsea, Everton, Real Madrid, Inter Milan, miongoni mwa nyingine ughaibuni, ni Mwafrika aliye na ushawishi mkubwa mno.

Sawa na wafanyavyo watu wengine wengi mashuhuri wanapozuru nchini, mwanaspoti huyo ambaye hivi sasa ni rais wa Shirikisho la Kandanda Cameroon alitalii Malindi kwa usiri mkubwa mno.

Hii inaeleweka kwa vile wanapoonekana hadharani, watu mashuhuri hukumbwa na usumbufu mwingi unaoweza kutatiza hitaji lao la mapumziko.

Hata hivyo, wadau wa sekta ya utalii walikosa nafasi mwafaka ya kutumia ziara yake nchini kueneza habari kimataifa kuhusu utalii Pwani.

Wakati mwingi huwa tunasikia malalamishi kutoka kwa waekezaji wa utalii kwamba sekta hiyo inadorora, na wito wao mkuu huwa ni kwa serikali kuingilia kati.

Lakini inafaa itambulike kuwa, kuna mambo mengi ambayo wadau wenyewe wanaweza kufanya ili kuongezea zile juhudi zinazofanywa na serikali kufufua sekta hiyo.

Enzi hizi za teknolojia za mawasiliano zimetoa nafasi tele ambazo zinaweza kutumiwa kueneza hamasisho kuhusu suala lolote lile.

Huenda ikawa Eto’o hakutaka kufuatiliwa sana wakati wa ziara yake na familia yake humu nchini, lakini mtaalamu yeyote wa mawasiliano hangekosa njia ya kutumia ziara hiyo kuhakikisha watu wanapomzungumzia mchezaji huyo, wanapata pia habari kuhusu Malindi katika kipindi ambapo gumzo kumhusu lilikuwa likiendelea.

Hii si mara ya kwanza ambapo nafasi kama hii imeachwa ikapotea bila wadau kuitumia kuvumisha Pwani kimataifa.

Takriban miaka mitatu iliyopita, mwigizaji Mkenya anayetamba kimataifa, Lupita Nyong’o, aliibua gumzo mitandaoni alipoeleza kuhusu ziara yake Lamu.

Hatukuona wadau wa utalii wakishabikia ziara hiyo yake kutangaza utalii wa Lamu.

Matukio mengine mengi ya kuvutia yamewahi kushuhudiwa, ila huachwa kutokomea bila kutiliwa uzito.

Wadau wa utalii wajiondolee mawazo kuwa kutangaza maeneo ya kuvutia nchini kunahitaji mamilioni au hata mabilioni ya pesa, bali watumie vyema kila nafasi inayoibuka kufufua sekta hiyo inayoshuhudia changamoto.

 

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Ulimwengu wa Kiswahili waenzi mwandishi...

Jesse Lingard aamua kuondoka Man-United mwishoni mwa msimu...

T L