• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
NGUVU ZA HOJA: Matunda ya kwanza kabisa ya mtaala mpya wa umilisi yatabainika mwaka huu

NGUVU ZA HOJA: Matunda ya kwanza kabisa ya mtaala mpya wa umilisi yatabainika mwaka huu

NA PROF JOHN KOBIA

MTAALA wa umilisi umepiga hatua katika utekelezaji wake kwani wanafunzi wa kwanza katika mfumo huu katika shule za msingi, wameingia Gredi ya Sita muhula huu.

Tathmini ya kwanza ya gredi ya Sita inatarajiwa kufanywa mwaka huu. Kuanzia mwaka ujao (2023) wanafunzi hao wataingia gredi ya saba ambayo ndio mwanzo wa daraja ya awali ya shule za upili.

Binadamu huhitaji kujieleza kwa kutumia lugha katika miktadha mbalimbali. Mwanafunzi katika daraja ya awali (kuanzia gredi ya 7 hadi 9) katika shule ya upili anatarajiwa kujieleza ipasavyo kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa maandishi na mazungumzo.

Umilisi wa kujieleza unatarajiwa kukuzwa kupitia njia mbalimbali kama vile kusikiliza na kujibu mazungumzo, hotuba, matamshi bora na kuimba nyimbo mbalimbali.

Vilevile, umilisi wa kujieleza kwa Kiswahili unakuzwa kupitia kuandika barua kama za kirafiki, rasmi, baruapepe, kuandika insha za maelezo, masimulizi na wasifu.

Isitoshe, mtaala wa kiumilisi unamtarajia mwanafunzi awe na uwezo wa kujenga desturi ya kusoma na kufasiri maandishi kwa ufasaha.

Mwanafunzi anatarajiwa kuchangamkia usomaji wa vifungu mbalimbali, novela, kamusi, tamthilia, mashairi, majarida, magazeti na matini kwenye tovuti.

Kwa kufanya hivi, talanta ya mwanafunzi itatambulika mapema na kumwaandaa kuchagua uwanja wa kazi anaotazamia kuzamia.

Inatarajiwa kuwa kufikia mwisho wa daraja ya awali katika shule ya upili, mwanafunzi atakuwa na uwezo kutumia lugha ya Kiswahili kibunifu kusimulia na kuandika tungo mbalimbali.

Mwanafunzi ataweza kutumia Kiswahili kuandika tungo za kibunifu kama vile mashairi mepesi, nyimbo, hadithi fupi, novela.

Pia, atasimulia ngano, kutaja methali na kutega na kutegua vitendawili.

  • Tags

You can share this post!

DCI wachunguza bunduki iliyoua mtoto wa mbunge

NGUVU ZA HOJA: Ulimwengu wa Kiswahili waenzi mwandishi...

T L