• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
NGUVU ZA HOJA: Walimu wa lugha ya Kiswahili waandaliwe vyema kwa ajili ya Mtaala wa Kiumilisi (CBC)

NGUVU ZA HOJA: Walimu wa lugha ya Kiswahili waandaliwe vyema kwa ajili ya Mtaala wa Kiumilisi (CBC)

NA PROF JOHN KOBIA

WANAFUNZI wa gredi ya saba wanatarajiwa kuanza masomo yao ya sekondari ya awali Jumatatu wiki ijayo.

Hawa ni wanafunzi waliofanya tathmini tamati ya KPSEA mwaka 2022. Kuna changamoto nyingi zinazokumba utekelezaji wa Mtaala wa Kiumilisi (CBC).

Mojawapo ya changamoto katika utekelezaji wa mtaala huu ni maandalizi finyu ya walimu wa Kiswahili. Walimu ni muhimu katika ufanisi wa utekelezaji wa mfumo wa elimu. Walimu hufasiri na hutekeleza mtaala wa kiumilisi.

Ingawa walimu wa Kiswahili wamepata mafunzo hapa na pale kuhusu utekelezaji wa mtaala huu mpya, bado mafunzo zaidi yanahitajika.

Kwa sababu Kiswahili ni mojawapo ya masomo ya lazima katika gredi ya saba, muda wa kutoa mafunzo kwa walimu wa Kiswahili unapaswa kuongezwa ili waweze kumakinika zaidi katika nyanja mbalimbali za utekelezaji wa CBC.

Maandalizi mwafaka ya walimu ni muhimu katika utekelezaji. Mtindo wa kutoa mafunzo ya wiki moja kwa masomo yote kijumla haufai.

Mafunzo ya walimu yanapaswa kutolewa kwa kipindi cha wiki mbili au zaidi kila likizo.

Mafunzo haya yazingatie mada, mada ndogo, matokeo maalumu yanayotarajiwa na maswali dadisi katika kila mada.

Mafunzo ya walimu wa Kiswahili pia yalenge mapendekezo ya hatua za ufunzaji na ujifunzaji, umilisi wa kimsingi unaokuzwa, maadili yanayokuzwa, masuala mtambuko na uhusiano wa mada za Kiswahili na masomo mengine.

Walimu wa Kiswahili pia waandaliwe kuhusu nyenzo, tathmini na mbinu za kufundisha Kiswahili katika kiwango hiki.

Maandalizi mwafaka ya walimu wa Kiswahili yatachangia ufanisi wa utekelezaji wa mtaala wa kiumilisi.

  • Tags

You can share this post!

Aliyekuwa mpuliza kipenga wa EPL, Mark Clattenburg,...

Mrembo aliyeegesha gari katikati ya barabara kupokea busu...

T L