• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
NJENJE: Afueni kwa wafugaji serikali ikitangaza kuondoa ushuru kwa mahindi ya manjano

NJENJE: Afueni kwa wafugaji serikali ikitangaza kuondoa ushuru kwa mahindi ya manjano

NA WANDERI KAMAU

WIZARA ya Kilimo imewaruhusu watu wanaotengeneza vyakula vya mifugo kuagiza tani 350,000 za mahindi ya manjano bila kutozwa ushuru wowote kwa muda wa mwaka mmoja ujao, ili kudhibiti bei za juu kwa sasa.

Kwenye kikao na Chama cha Watengenezaji Lishe ya Mifugo (Akefema) wiki iliyopita, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi alisema kuwa serikali itachukua hatua hiyo ili kukabili uhaba uliopo wa mahindi ya kawaida.

“Serikali itaondoa ushuru unaotozwa mahindi ya manjano yanayotumika kama lishe ya mifugo kwa muda wa mwaka mmoja ujao,” akasema Bw Linturi.

Agizo hilo linajiri miezi miwili baada ya muda uliokuwa umewekwa kuruhusu uagizaji wa mahindi aina hiyo bila kutozwa ushuru kukamilika.

Kama njia ya kutafuta suluhisho la kudumu, Bw Linturi aliwarai watengenezaji hao kuunga mkono mkakati wa kilimo wa upanzi wa bidhaa za kutengeneza vyakula vya mifugo, ili kupunguza gharama wanayotumia kuagiza vyakula hivyo kutoka nchi za nje.

Wiki iliyopita, serikali pia ilitangaza kuruhusu uagizaji wa mahindi ya kawaida ili kudhibiti uhaba wa zao hilo nchini.

Upungufu wa mahindi hayo nchini umechangia bei ya unga kupanda, licha ya ahadi ya serikali kuipunguza.

Wasagaji walioagiza mahindi hayo kati ya Juni na Septemba walilazimika kukaa nayo baada ya kukosa kupata soko.Wasagaji walikuwa wameagiza mahindi hayo kwa matumizi yao binafsi na kuwauzia watengenezaji wa kiwango cha chini ambao hawakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha kuyaagiza.

Hata hivyo, wasagaji hao walishindwa kuuza mahindi hayo, ikizingatiwa kuwa gunia moja la kilo 90 la mahindi ya manjano lilikuwa likiuzwa kwa Sh5,600 huku gunia moja la mahindi ya kawaida likiuzwa kwa Sh5,300.

Mwenyekiti wa Akefema, Bw Joseph Karusi, anasema kuwa bei za zao hilo duniani zimeshuka, hivyo kuna uwezekano watauziwa kwa bei za chini ikilinganishwa na hapo awali.

“Bei za mahindi ya manjano zinaimarika. Hivyo, tunatarajia kuyanunua kwa bei nzuri zitakazochangia gharama ya vyakula vya mifugo kupungua kufikia Februari mwaka ujao,” akasema Bw Karuri.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Huduma za arafa zimemjengea jina

MITAMBO: Ni afueni mfumo wa kuunda bayogesi ukikata gharama

T L