• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
UJASIRIAMALI: Huduma za arafa zimemjengea jina

UJASIRIAMALI: Huduma za arafa zimemjengea jina

NA PETER CHANGTOEK

ALIPOJIWA na wazo la kuianzisha kampuni yake, Robert Lang’at hakuwa na fedha za kutosha, na ilibidi aongezewe na marafiki.

Isitoshe, hakuwa hata na afisi ya kufanyia shughuli zake, na ikabidi apewe sehemu ndogo na rafiki yake mmoja, karibu na barabara ya Ngong.

Alianzisha kampuni inayojulikana kama Mobitech Technologies Limited, inayotoa huduma za arafa kwa wingi kwa wateja kwa bei nafuu.

Lang’at aliistawisha kampuni hiyo, hadi wakati huu ambapo ana wafanyakazi watano katika eneo la Westlands, anakoendesha shughuli zake, na huwahudumia zaidi ya wateja 1,000.

“Niliianzisha kwa akiba niliyokuwa nayo, pamoja na mchango kutoka kwa marafiki. Nilianza kwa kufanya kazi nikiwa nyumbani, huku nikiwapata wateja kadhaa. Baadaye, nikapata leseni zinazohitajika na kuhamia afisi zetu,” aeleza Lang’at, akiongeza kuwa, walihamia afisi zao za Westlands 2013.

Baadaye alianza kupata wateja waliokuwa wakitumwa kwake na wale waliowahi kuzitumia huduma zake na kuridhishwa nazo.

“Tulianzisha Mobitech Technologies 2012, hapo ndipo kampuni iliposajiliwa na kuanza kufanya kazi. Tumesajiliwa na CAK. Tunatoa huduma za arafa kupitia kampuni tofauti za mawasiliano kama vile Safaricom na Airtel,” aongeza mjasiriamali huyo.

Lang’at, ambaye ni mhandisi wa mawasiliano, alikuwa ameajiriwa hapo awali kubuni apu za simu.

Alipokuwa akihudumu, akaona pengo katika utoaji wa huduma za arafa, na nafasi hiyo ikamletea biashara, alipoanzisha kampuni yake.

Anafichua kuwa, kampuni yake hushirikiana na kampuni za Safaricom, Airtel na Telkom Kenya, kutoa huduma za arafa kwa wingi kwa bei nafuu.

“Tulianza kwa kuwapa wateja huduma bora na kuwaonyesha uhusiano mwema. Tunawatengenezea wateja akaunti na wao ndio huzidhibiti kikamilifu; kwa mfano, hufungua akaunti na kuweka anwani zao na kuwatumia arafa (SMS),” asema.

Anadokeza kuwa, wengi wa wateja wao ni taasisi mbalimbali kama vile shule na vyuo.

Mbali na shule na vyuo, wao pia hutoa huduma zao kwa vyama vya ushirika, makanisa, watoaji huduma za mitandao, makasino, supamaketi na asasi za serikali kama vile ISK.

Aidha, hutoa huduma zao kwa kampuni za kujenga na kuuza nyumba na mashamba, makundi mbalimbali, hospitali pamoja na kampuni za kamari.

Ili kutumia huduma zao, mja anafaa kuwa na simu ya kisasa.

Hata hivyo, Lang’at anashauri kuwa, ni bora kutumia kompyuta au kipakatalishi.

Anawashauri wale ambao wana nia ya kujitosa katika biashara kama hiyo kujiamini na kuwapa wateja wao huduma bora.

“Hutoza ada ya Sh0.35 kwa arafa moja kwa mitandao yote. Hatutozi ada za kila mwezi au za usajili. Arafa zetu zilizonunuliwa hazina muda wa kuchina. Hutoza Sh6,800 mara moja kwa jina la kutumia na kwa kila kampuni ya mawasiliano,” asema Lang’at.

Mjasiriamali huyo anasema kuwa, wanapania kutoa huduma zao nchini Uganda na Tanzania na hata barani Afrika. Pia, wanapania kueneza huduma zao nje ya Nairobi na kuhudumu katika kaunti nyinginezo nchini.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Nguruwe wampatia maisha mapya baa iliposambaratika

NJENJE: Afueni kwa wafugaji serikali ikitangaza kuondoa...

T L