• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
NJENJE: Rwanda sasa yaipita Kenya kwenye bei bora za majanichai

NJENJE: Rwanda sasa yaipita Kenya kwenye bei bora za majanichai

NA WANDERI KAMAU

MAJANICHAI kutoka Rwanda yanaendelea kununuliwa kwa bei ya juu katika soko la kuuzia mazao la Mombasa, ikilinganishwa na zao hilo kutoka mataifa mengine kama Kenya.

Wanunuzi wengi wanasifia majanichai hayo kuwa yenye ubora wa kiwango cha juu, ikilinganishwa na yale yanayozalishwa katika maeneo mengine ukanda wa Afrika Mashariki.

Kulingana na takwimu za mauzo kutoka soko hilo, kilo moja ya majanichai ya Rwanda yananunuliwa kwa Sh326, ikilinganishwa na kiwango sawa kutoka Kenya, kinachouzwa kwa Sh292.

Katika nchi za Tanzania na Uganda, majanichai hayo yanauzwa kwa Sh174 na Sh165 mtawalia.

Bei za majanichai kutoka Rwanda zimekuwa zikiongoza katika soko hilo kwa muda mrefu ikilinganishwa na aina nyingine, yakisifiwa kwa ubora wa kipekee.

Ni hali ambayo imekuwa ikiizalishia Rwanda pato kubwa kinyume na mataifa mengine.

“Majanichai ya Rwanda huwa yana ladha ya kipekee ambayo huwavutia sana watumiaji wake. Hilo ndilo limeyafanya kuendelea kuongoza kwenye mauzo yake sokoni,” akasema dalali mmoja kwenye soko hilo.

Kiwastani, majanichai yaliuzwa kwa Sh277 kwa kilo moja wiki iliyopita, kiwango ambacho ni ongezeko la Sh3 (yalinunuliwa kwa Sh274 wiki liyotangulia).

Majanichai hayo yanajumuisha yale yanayozalishwa na wakulima wadogo wadogo nchini, mashirika ya kimataifa na mataifa mengine matano ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Nchi hizo zote huuza majanichai yao kupitia soko la Mombasa.

Majanichai hayo huuzwa kwanza katika soko hilo kupitia Chama cha Wauzaji Majanichai cha Afrika Mashariki (EATTA) kabla ya kusafirishwa nje ya nchi ili kuuzwa ng’ambo.

“Ijapokuwa Kenya inazidi Rwanda pakubwa kutokana na kiwango cha majanichai inayozalisha, ni hali inayofaa kuwafungua macho wadau nchini kuwa, si vigumu Kenya kupitwa na taifa jingine kwenye uzalishaji iikiwa watakosa kuweka mikakati ifaayo,” asema mwanauchumi, Bw Tony Watima.

  • Tags

You can share this post!

KCPE 2022: Mwanafunzi bora kote nchini apata alama 431

MITAMBO: Mashini inayosaidia kupakia mazao na kuyahifadhi...

T L