• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
NLC yalalamikia mgao finyu wa fedha inazopokea kutoka kwa serikali

NLC yalalamikia mgao finyu wa fedha inazopokea kutoka kwa serikali

Na SAMMY WAWERU

TUME ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) imelalamika kwamba inapokea mgao wa chini kabisa wa fedha kutoka kwa serikali, ikisema hauwezi kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa njia inayostahili.

NLC imesema uhaba wa pesa unamaanisha huduma za mashamba na umiliki wa vipande vya ardhi nchini ni duni.

Huku mwaka wa kwanza kuafikia mikakati yake kwenye mipango ya utendakazi 2021 – 2026 ukihitaji kima cha Sh3.6 bilioni, tume hii inasema imekabidhiwa Sh87 milioni pekee.

“Kwa mujibu wa mgao tuliopata, tuna upungufu wa Sh3.5 bilioni, na pengo hili litatatiza utendakazi wetu,” akalamika mwenyekiti wa NLC, Bw Gershom Otachi.

Afisa huyo hata hivyo alisema tume yake inaendelea kujadiliana na Hazina ya Kitaifa na bunge kuona iwapo itapata nyongeza ya fedha.

“Janga la Covid-19 pia limeathiri utoaji huduma za mashamba, hasa wakati wa amri ya ama kuingia au kutoka kaunti zilizokuwa zimewekewa marufuku,” akasema.

Bw Otachi alisema hayo kwenye hafla iliyoandaliwa na NLC jijini Nairobi, ili kueleza mipango ya utendakazi wake kipichi cha miaka mitano ijayo kutoka sasa.

Alitoa malalamiko ya NLC huku muda wa makataa ya kuwasilisha mizozo ya ardhi ukikaribia.

Septemba 21, 2021 ndiyo siku ya mwisho kwa wenye vipande vya ardhi na mashamba yenye historia ya mizozo, kuwataka wawe wamewasilisha malalamishi yao.

Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) inalalamikia mgao wa chini wa fedha inaopokea kutoka kwa serikali unakwamisha utendakazi wake. Picha/
Sammy Waweru

NLC hata hivyo inasema ingali na muda kushughulikia kesi itakazopokea.

“Baada ya makataa kuwasilisha malalamishi ya ardhi na mashamba yenye historia za mizozo kukamilika, tutakuwa na muda wa kutosha kuyashughulikia,” Bw Otachi akaelezea.

Alisema kufikia sasa, tume imepokea jumla ya kesi 740 kutoka maeneo tofauti ya nchi.

Kati ya kesi hizo, 395 zimesajiliwa, 340 zikiendelea kuchunguzwa na zilizosikilizwa na kuamuliwa zikiwa 126.

Alidokeza kwamba, kesi 5 zinaendelea kusikilizwa.

Bonde la Ufa linaongozwa kwa malalamishi 360, likifuatwa na eneo la Kati 114 na Pwani 101.

Huku mizozo ya ardhi na mashamba ikiendelea kuzua uhasama kati ya jamaa na jamii nchini, baadhi ya wahusika wajikipata kupigana na hata wengine kujeruhiana na kuuana, NLC inasema malalamishi iliyopokea kutoka sehemu zote za nchi yanawiana.

Tume hiyo inaeleza yanahusisha mizozo ya kuanzia siku za ukoloni, ukosefu wa usawa katika ugavi wa mashamba, wamiliki kukosa kukabidhiwa hatimiliki, mivutano ya raslimali, wamiliki halali kuondolewa kwa nguvu na wanyakuzi wa ardhi na mingine kusababishwa na majanga asili.

You can share this post!

‘Uganda ni mwalimu wa jinsi Kenya ilifaa kukaribisha...

SUPER CUP: Tammy Abraham kuongoza mashabulizi ya Chelsea...