• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
‘Uganda ni mwalimu wa jinsi Kenya ilifaa kukaribisha wanariadha’

‘Uganda ni mwalimu wa jinsi Kenya ilifaa kukaribisha wanariadha’

Na GEOFFREY ANENE

WAZIRI wa Michezo Amina Mohamed pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wamekashifiwa vikali kwa kutojitokeza katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kupokea shujaa Eliud Kipchoge aliyewasili nchini usiku wa kuamkia Jumatano kutoka Japan alikohifadhi taji la Olimpiki la marathon.

Kenya ilikamilisha mashindano hayo katika nafasi ya 19 duniani na nambari moja Afrika kwa kuzoa dhahabu nne, fedha nne na shaba mbili.

Kilichoudhi Wakenya hata zaidi ni kuwa timu ya Uganda, ambayo iliambulia dhahabu tatu pekee ikimaliza kampeni yake katika nafasi ya 39, ilipokelewa kishujaa na Rais Yoweri Museveni.

Mshikilizi wa rekodi ya marathon ya wanaume Kipchoge aliwasili pamoja na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 Ruth Chepng’etich na bingwa wa dunia mbio za mita 1,500.

Haya hapa maoni ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhusu tofauti kubwa ya mapokezi ya Team Kenya na wenzao kutoka Uganda baada ya kuanzishwa kwa #AsanteCSAmina:

EDWARD{MR.POLITICIAN} (@EdwardOmwansa) – “Huu ni upuuzi mtupu. Wanamichezo wetu wa Kenya wanawasili kama wezi…”

Gilbert Ngenoh (@GilbertNgenoh) – “Serikali ya Uganda inatambua wanariadha wao, waziri wetu hapa anajisifu kupitia kwa mtandao. Mungu awepende wanariadha wetu na tunawapenda, Faith Kipyegon, Eliud Kipchoge… Serikali ya Kenya inafaa kuvunjwa. #AsanteCSAmina aibu, aibu… hebu ona jinsi Uganda inakaribisha wanariadha wao, huku wetu wakirejea nchini kama washindi wasiotakikana…inasikitisha.”

Maurice Diyah (@MauricediyahWes) – “Wanariadha wetu wanaendelea kuwasili kutoka Tokyo bila sisi kujua. Hakuna hata mtu mashuhuri wa kuwakaribisha, hata baada ya kazi nzuri kutoka kwa mashujaa wetu.”

Tunen Titus (@TunenKe) – “Wanamedali wa Uganda kutoka Japan wamekaribishwa na Rais Museveni katika uwanja wa Kololo. Hapa Kenya, timu yetu ya Olimpiki inawasili na kuelekea katika kituo cha basi kuabiri gari la kuelekea Chepalungu. #AsanteCSAmina. Inasikitisha, ni aibu kubwa na inavunja moyo kushuhudia mapokezi haya baridi dhidi ya mashujaa wetu.

Kibiro Peter (KibiroPeter) – “Wanariadha wetu wamewasili nyumbani kama wanyama wasiotakikana. Wanaendelea kuwasili bila kutambuliwa wala kupokelewa. Hii inafanyika huku ndugu zetu wakubwa wakiwa hawa muda nao kwa sababu wamezamia kupanga uchaguzi wa 2022. Aibu sana!”

Lord Abraham Mutai (@ItsMutai) – “Hivi ndivyo wanariadha wa Kenya waliwasili. Hata watu waliokuwa katika uwanja wa ndege waliwatazama na kushangaa kukosekana mapokezi. Kusema inasikitisha bado haitoshi. Walifanya vyema, walirejea kimyakimya, bila ya kupokelewa, lakini tukiamka leo asubuhi, tunapata ujumbe kwenye mtandao wa Twitter wa kushukuru Waziri wa Michezo #AsanteCSAmina.”

Saddique Shaban (@SaddiqueShaban) – “Uongozi wa Wizara ya Michezo umeacha wanaolimpiki wa Kenya kama Eliud Kipchoge kuhangaika katika uwanja wa ndege jijini Nairobi. Hakuna mapokezi, hakuna chochote, licha ya gwiji huyo na wengine kufanya dunia nzima inyanyuke kwa heshima ya wimbo wetu wa taifa kwenye Olimpiki za Tokyo 2020.”

Denis Mutahi (@ItsMutaiKE) – “Aibu kwako Rais Uhuru Kenyatta na Waziri wa Michezo Amina Mohamed.”

You can share this post!

Mwanasiasa mkongwe George Nthenge afariki

NLC yalalamikia mgao finyu wa fedha inazopokea kutoka kwa...