• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Nzi aina ya BSF kupunguza gharama ya ufugaji kuku

Nzi aina ya BSF kupunguza gharama ya ufugaji kuku

NA SAMMY WAWERU

ENEOBUNGE la Gatanga, Kiambu ni lenye shughuli nyingi za kilimo na ndiko Margaret Macharia anaendeleza ufugaji wa kuku. 

Hufuga kuku walioboreshwa wa kienyeji, na mbali na ndege hao, Margaret na mumewe pia wanashiriki ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kuyaongeza thamani.

Vilevile, hufuga samaki, shughuli zote hizo wakizifanya kwenye nusu ekari.

Mama huyu ambaye ni Naibu Chifu Mtaa wa Golf View, aliingilia ufugaji kuku mwaka 1990, ili kujipa pato la ziada.

Ufugaji kuku umekuwa biashara yenye faida, japo Margaret anasema miaka mitatu iliyopita mambo yalianza kuenda mrama.

Wafugaji wa kuku wanazidi kulemewa na bei ya juu ya chakula cha madukani, mfumko wa bei ulioanza kushuhudiwa Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa janga la ugonjwa wa Covid-19 mwaka 2020.

Margaret Macharia, mfugaji wa kuku Murang’a anayetumia BSF kupunguza gharama ya malisho. PICHA|SAMMY WAWERU

Kenya na ulimwengu, hata hivyo, sasa ni huru dhidi ya maradhi hayo yaliyosababishwa na virusi vya Corona.

“Kabla ya ugonjwa huo kutua nchini, vyumba vyangu vya kuku vilikuwa vimejaa ila sasa kwa sababu ya ughali wa malisho mambo yamebadilika kabisa,” Margaret anasema.

Kipande cha godoro kilicholoweshwa maji ili BSF kuyafyonza. PICHA|SAMMY WAWERU

Mfugaji huyu anakumbuka awali biashara yake ikichezea kati ya kuku 3, 600 kwa wakati mmoja.

Kwa sasa, anasema idadi anayofugaji ni wastani wa 500 “chakula cha madukani kikiwa ndio sababu ya punguo hilo la juu”.

Sekta ya kuku imeathirika pakubwa kutokana na ongezeko la bei ya chakula cha mifugo, ikikadiriwa Kenya huagiza zaidi ya asilimia 70 ya malighafi yanayotumika kukiunda.

Wadudu aina ya BSF ambao Margaret Macharia, mfugaji wa kuku Murang’a anatumia kupunguza gharama ya malisho. PICHA|SAMMY WAWERU

Malighafi ya chakula cha mifugo ni pamoja na mahindi, ngano (wheat bran), shayiri, soya, mbegu za pamba, miongoni mwa bidhaa zingine.

Kusalia kwenye biashara ya kuku, Margaret amevumbua nzi maalum – Black Soldier Flies (BSF) ni mbinu mwafaka kupunguza gharama ya uzalishaji.

BSF inasifiwa kuwa na kati ya asilimia 40 hadi 45 ya virutubisho vya Protini.

Ni nzi – wadudu aliotambua matumizi yake kupitia mafunzo katika Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) mwaka uliopita, 2022.

“Hatua hiyo tuliichukua baada ya kusimamisha ufugaji kuku Aprili 2022 na kuzamia utafiti uliotuelekeza JKUAT,” Margaret adokeza.

Aidha, mafunzo yalichukua siku moja pekee wakilipia ada ya Sh5, 000.

Margaret pia anadokeza kwamba walinolewa makali kuhusu ufugaji BSF kupitia Mpango wa Kuboresha Kilimo (ASDSP) Murang’a.

Margaret Macharia anasema alipata mafunzo ya BSF kutoka JKUAT. PICHA|SAMMY WAWERU

Vidimbwi vitatu walivyotumia kufuga samaki wamevigeuza kuwa ‘vizimba’ – cages kufuga nzi hao wenye thamani.

Sakafu na kuta, vidimbwi hivyo vimeundwa kwa sarufi kisha vikaezekwa kwa mabati na vizimba vyenyewe kwa mbao na nyavu.

Aidha, Margaret anatumia mitungi ya maji iliyogawanywa mara mbili kujamiisha na kuzalisha BSF.

Chakula cha wadudu hao ni masalia ya chakula cha binadamu, maganda ya matunda na kinyesi cha kuku, hatua inayofanya ufugaji wake kuwa nafuu na wa gharama ya chini.

Margaret anakadiria amepunguza gharama ya ufugaji kuku kwa karibu asilimia 40.

“Muhimu pia ni maji ambayo huyaweka kwenye mitungi yenye vipande vya magodoro vilivyoloweshwa wayafyonze,” Margaret akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano.

Mtaji aliotumia, anafichua kwamba ni Sh10, 000 pekee kupitia ununuzi wa BSF kilo moja akiuziwa na JKUAT Sh1, 000.

Aidha, nzi hao hutagia mayai kwenye vipande vya mbao vilivyowekwa pamoja na mlo ili kuendeleza kizazi kupitia uanguaji.

Huwapa kuku asilimia 80, kisha asilimia 20 iliyosalia anairejesha kwa minajili ya uzalishaji zaidi.

Margaret hufuga kuku aina ya rainbow rooster, kuroiler, na sasso.

  • Tags

You can share this post!

Peter Salasya: Mbunge aliyesheheni vituko japo mchapakazi

Mtaalamu – Wafugaji wakumbatie mbinu mbadala kushusha...

T L