• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Peter Salasya: Mbunge aliyesheheni vituko japo mchapakazi

Peter Salasya: Mbunge aliyesheheni vituko japo mchapakazi

NA SHABAN MAKOKHA

MBUNGE wa Mumias Mashariki Peter Kalerwa (PK) Salasya amekuwa akivuma kwa sababu tofauti tangu achaguliwe kuwa mbunge Agosti 9, 2022.

Jina lake limesalia kwenye midomo ya Wakenya kutokana na mazungumzo yake yasiyoisha kushika vichwa vya habari kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vikuu vya habari.

Lakini PK Salasya ni nani?

Mbunge huyu hajawahi kukwepa kusimulia safari yake ya kupanda hadhi, hata inapojaa utata. Ni mtu anayependwa na kuchukiwa kwa mizani sawa.

Alizaliwa katika kijiji cha Eluche, Mumias Mashariki katika Kaunti ya Kakamega Januari 1989.

Mbunge huyu alihudhuria Shule ya Msingi ya Shanderema kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Lubinu katika Kaunti ya Kakamega 2006.

Baba yake alifariki alipokuwa kidato cha pili na alisaidiwa na kaka yake mkubwa kupata elimu yake ya sekondari na chuo kikuu.

Baada ya Kidato cha Nne, alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton katika Kaunti ya Nakuru kusomea Shahada ya Kwanza ya Biashara.

Alianza siasa za chuo kikuu akiwa katika mwaka wa kwanza. Aliwania nafasi ya Mkurugenzi wa shughuli za masomo.

Hata hivyo, alishindwa na akafanya jaribio la pili katika mwaka wake wa tatu, mara hii akigombea nafasi ya makamu mwenyekiti lakini akashindwa tena.

Mnamo 2014, alihitimu na kurudi nyumbani ambapo alipata kazi yake ya kwanza kama mchuuzi akifanya biashara ya ndani ya kuuza baiskeli.

Kupitia usaidizi wa rafiki yake, Bw Salasya alipata kazi ya hadhi katika benki ya DTB mjini Kakamega, huku akiendelea kuwa na hamu ya kuwa kiongozi.

Baadaye alishiriki kwa mara ya kwanza katika siasa za kitaifa mnamo 2017 kwa kuwania kiti cha ubunge cha Mumias Mashariki.

Aliibuka wa mwisho kati ya wagombea tisa, akiwa na kura 254 pekee.

Baada ya uchaguzi, alipoteza kazi yake katika benki ila sasa akajitolea kuwa mwalimu katika Chuo cha Ufundi cha Kitaifa cha Sigalagala mshahara wake ukiwa Sh13, 000 kwa mwezi.

Alitumia sehemu ya pesa hizi kutangaza azma yake ya kisiasa.

Alianza kushughulika na suala la ufufuaji wa kampuni ya sukari ya Mumias, akipigania kununuliwa kwa mashine za kusaga miwa ili kuinusuru isiporomoke jambo ambalo lilimfanya achangamkiwe na wapigakura.

Katika uchaguzi wa 2022, Salasya alionekana kupendwa na watu wengi wa Mumias Mashariki, lakini hakuwa na rasilimali za kufanya kampeni.

Aliandika jina lake kwenye mawe katika eneobunge hilo kwa sababu hakuwa na uwezo wa kuchapisha mabango ya kampeni.

Bila mke na nyumba, wapigakura wake walijitolea kumjengea nyumba ya udongo kabla ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa kumuunga mkono kubadilisha jengo hilo kuwa la kudumu.

Bw Wamalwa baadaye alifadhili sehemu ya kampeni zake kwa sababu aligombea kwa tiketi ya chama chake (cha Wamalwa) cha DAP-K.

Bila rasilimali za kutosha hata kuajiri maajenti, Salasya alitegemea sana wafuasi kulinda kura zake, na kweli matokeo yalipotangazwa, alishinda.

Mbunge huyo amekuwa na vituko vingi na yaelekea hayuko tayari kuviacha. Tangu alipoapishwa kuwa mbunge, PK Salasya amekuwa akitajwa mara kwa mara kwa sababu nyingi, na kujijengea jina kupitia mabishano ndani na nje ya bunge.

Mara tu baada ya kuwa mbunge, Salasya alitangaza kwa umma sifa za mke ambaye alikuwa akitafuta kuoa.

Alizungumza kuhusu mwanamke msomi mwenye umri wa kati ya miaka 23-26 na ambaye asingeshika simu yake ya rununu, kama baadhi ya sifa alizokuwa akitafuta kwa mwanamke wa kuoa.

Alisema: ‘Pia anapaswa kuwa tayari kukaa kijijini, akichunga eneobunge.”

Mnamo Februari, 2023, aliibua mjadala mkali alipotoa matamshi ambayo wengi waliyaona kuwa ya kudhalilisha kingono kuhusu Mwakilishi wa Mwanamke wa Bomet Linet Chepkorir almaarufu Toto.

Salasya alimkashifu mwakilishi huyo wa wanawake kwa kutomheshimu kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.

“Kati ya vijana wanaomdhulumu Baba, kuna mmoja ambaye alipigiwa kura lakini hakuwa na pesa kama Peter Salasya. Anaitwa Toto. Nitaenda kumpa ujauzito wiki ijayo,” mbunge huyo alisema kabla ya kuomba radhi kwa kauli yake na kuridhiana na Toto.

Muda mfupi baadaye, alikuwa akimulikwa tena kwa matamshi yake pembezoni mwa Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi Barani Afrika lililofanyika katika Jumba la Mikutano la Kenyatta (KICC), Jijini Nairobi wakati alionekana kutofahamu vyema masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Baadaye aliwapuuza waliomkosoa akisema kazi yake haihusu Mabadiliko ya Tabianchi, bali masuala yanayohusu watu wa Mumias Mashariki.

Salasya akiwa mkosoaji mkali wa Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, alizua mtafaruku mwingine kabla ya vijana washirika wa Bw Barasa kumvamia na kumfukuza kutoka kwenye hafla ya kanisa eneo la Bukaya, Mumias Magharibi.

Bw Salasya alikuwa akizungumzia masuala yanayoathiri ufufuzi wa Kampuni ya Sukari ya Mumias wakati mwanamume mmoja mshirika wa mkuu huyo wa kaunti alipompokonya kipaza sauti ili kukatiza hotuba yake.

Mapigano yalizuka na watu zaidi wakajiunga huku mwenyeji wa hafla hiyo, mbunge wa Mumias Magharibi Johnson Naicca na wageni wengine miongoni mwao Gavana Barasa, wakitazama kwa mshangao.

Walinzi wa Bw Salasya walilazimika kufyatua risasi hewani walipokuwa wakimuondoa mbunge huyo hadi eneo salama.

Kisa hicho kilijiri wiki moja tu baada ya wakili katika Kaunti ya Kakamega kumshtaki Salasya kwa madai ya kumshambulia na kumtusi.

Mbunge huyo anadaiwa kumshambulia wakili Edwin Wafula kwa sababu ya kesi ambapo anadaiwa (Salasya) kukosa kulipa mkopo wa Sh500, 000 aliopewa baada ya uchaguzi wa Agosti 2022.

Bw Wafula tangu wakati huo alienda kortini akimshutumu Salasya kwa kumshambulia na matusi mara mbili tofauti ndani ya mji wa Kakamega.

Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi Gladys Kiama.

Licha ya msururu wa vituko kumwandama, mbunge huyo anayehudumu muhula wa kwanza aliibuka miongoni mwa wabunge waliofanya vyema zaidi nchini katika utafiti wa hivi majuzi wa Infortrak.

Mapema mwezi huu, Novemba 2023, kura ya maoni iliorodhesha Bw Salasya pamoja na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na Naisula Lesuuda (SamburuWest) kuwa wabunge vijana waliofanya vizuri zaidi nchini Kenya.

Kura hiyo ya maoni ilimweka Bw Salasya katika nafasi ya nne kwa wastani wa asilimia 64 katika orodha ya wabunge 10 wachapakazi mwaka huu, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Baraza la Jamii ya Abagusii Nairobi lamkosoa Ruto kuhusu...

Nzi aina ya BSF kupunguza gharama ya ufugaji kuku

T L