• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
ODONGO: Ruto agutuke awateme wanasiasa wasiomfaa

ODONGO: Ruto agutuke awateme wanasiasa wasiomfaa

Na CECIL ODONGO

NAIBU Rais, Dkt William Ruto anafaa agutuke na kuwatema baadhi ya wandani wake hasa katika maeneo ya Magharibi na Ukambani baada ya wawaniaji wa chama cha UDA kushindwa vibaya katika chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai na ule wa Useneta wa Machakos.

Dkt Ruto amekuwa akihusishwa na chama hicho cha Wilbaro na ilidaiwa kwamba umaarufu wake ulikuwa umepanda kisiasa hasa eneo la Ukambani na Magharibi mwa nchi kabla ya chaguzi hizo ndogo.

Hata hivyo, sasa imebainika kwamba hana ufuasi wowote wa maana licha ya kuzuru maeneo hayo mawili mara kwa mara na kushiriki michango huku akijinadi kama mwaniaji bora zaidi kuingia ikulu mnamo 2022.

Katika chaguzi hizo tatu, UDA ilijizolea aibu zaidi kwenye kura ya Machakos ambapo mwaniaji wake Urbanus Ngengele alishindwa kwa zaidi ya kura 80,000 na Seneta mteule Agnes Kavindu Muthama wa Wiper.

Licha ya kampeni kali ya mwenyekiti wa UDA Johnstone Muthama, wabunge Victor Munyaka (Machakos Mjini), Vincent Musyoka ‘Kawaya’ (Mwala), Nimrod Mbai (Kitui Mashariki) kati ya wengine, upande wa Wiper uling’aa zaidi na kudhihirisha uaminifu wa wakazi wa eneo hilo katika uongozi wa makamu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka.

Magharibi mwa nchi, mwaniaji wa UDA Alex Lanya aliibuka wa tatu huku akishindwa kwa zaidi ya kura 10,000 na mshindi Peter Nabulindo wa ANC.

Hali ilikuwa hiyo katika uchaguzi mdogo wa Kabuchai, alishindwa kwa zaidi ya kura 13,000 na mshindi Majimbo Kalasinga wa Ford Kenya.

Katika eneo la Magharibi majemedari wa Dkt Ruto ni wabunge Ben Washiali (Mumias Mashariki), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Didmus Barasa (Kiminini), aliyekuwa seneta wa Kakamega Bonny Khalwale miongoni mwa viongozi wengine.

Matokeo haya yanafaa kumwaamsha Naibu Rais usingizini kwa kuwa viongozi anaowaamini katika maeneo ya Magharibi na Ukambani hawamvutii uungwaji mkono wowote wa maana katika maeneo hayo na mengine kote nchini.

Ingawa inaweza kudadisiwa kwamba muungano wa vyama vya Wiper, ANC na Kanu ulichangia kushindwa kwake vibaya, itakuaje muungano huo ukidumu hadi 2022 na abwagwe katika mbio za kuingia ikulu?

Naibu Rais anafaa awateme viongozi hao na afike nyanjani ili kutambua viongozi wanaoshabikiwa na raia moja kwa moja ili kuvumisha urais wake ikizingatiwa baadhi ya wandani wake kwa sasa hata walikataliwa na wapigakura mnamo 2017.

Ingawa ngome yake ya Bonde la Ufa ina wapigakura wengi, Dkt Ruto ana kibarua kuhakikisha kuwa injili yake inasikika hata maeneo ambayo ni ngome ya upinzani ili awe katika nafasi bora ya kutamba mwaka 2022.

You can share this post!

WARUI: Ni jukumu letu sote kuzuia wizi wa mitihani ya...

PATA USHAURI WA DKT FLO: Vidonda vya mafua huletwa na nini?