• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
ODONGO: Tiketi ya ODM: Oparanya, Joho wanajipumbaza tu!

ODONGO: Tiketi ya ODM: Oparanya, Joho wanajipumbaza tu!

Na CECIL ODONGO

MAGAVANA Ali Hassan Joho na Wycliffe Oparanya wanafaa wakome kujihadaa kuwa wanaweza kumbwaga Kinara wa ODM Raila Odinga katika juhudi za kusaka tiketi ya ODM ili kuwania Urais mwaka 2022.

Mabw Joho na Oparanya waliwasilisha majina yao kwa Bodi ya Uchaguzi wa ODM inayoongozwa na Dkt Catherine Mumma ambapo sasa imebainika kuwa watamenyana na Bw Odinga katika mchujo huo.

Kando na kuchaguliwa kwa tiketi ya ODM, wawili hao wanashikilia cheo cha Naibu Mwenyekiti wa chama na wamekuwa majemedari wa Bw Odinga kwa muda mrefu.

Kwanza, wanastahili pongezi kwa kutuma maombi ili chama kiwape nafasi ya kusaka uongozi wa nchi ila hata wao wenyewe wanafahamu bado hawatoshi mboga.

Mabw Oparanya na Joho ni wanasiasa ambao hawana ufuasi mkubwa ukilinganishwa na Bw Odinga ambaye sasa wafuasi wake wanaamini wakati wake umetimia baada ya kuanguka Urais mara tano. Imani yao inachochewa na ushirikiano kati ya kiongozi wao na Rais Uhuru Kenyatta kupitia handisheki.

Ndiyo, Bw Oparanya amejizolea sifa kama mwanasiasa mchapakazi tangu akiwa katika serikali ya muungano mnamo 2007 akisimamia wizara ya mipango ya kiuchumi na ruwaza ya 2030.

Akiwa gavana, Bw Oparanya ni kati ya wale walioorodheshwa kutokana na kuchapa kazi kwa njia inayoridhisha ndipo akashinda kipindi chake cha pili kwa urahisi mno.

Hata hivyo, mwelekeo wa sasa ambapo siasa za Magharibi zimeanza kuchukua zitamponza sura ya kitaifa na itakuwa vigumu sana apate tiketi ya ODM.

Kutoka eneo hilo hilo la Magharibi, Musalia Mudavadi wa ANC, Moses Wetang’ula wa Ford Kenya na waziri wa zamani Dkt Mukhisa Kituyi washatangaza kuwa wapo debeni mwaka ujao.

Kisiasa, Bw Mudavadi anaonekana kujizolea umaarufu eneo hilo na hilo linampa Bw Oparanya kibarua kigumu cha kuwashawishi wajumbe wa ODM wamuunge mkono ilhali nyumbani hashabikiwi.

Lau, mwaniaji wa ODM David Were angeshinda uchaguzi mdogo wa Matungu, Bw Oparanya angeonekana kama anayeimarika na kuwa kwenye kikoa kimoja na Mabw Mudavadi na Wetang’ula.

Pia isisahaulike kuwa Bw Odinga anashabikiwa sana Magharibi kuliko hata viongozi wa eneo hilo ambao wametangaza azma yao ya kuingia ikulu.

Kwa upande mwingine, Bw Joho bado ana safari ndefu kisiasa hasa kuwaunganisha Wapwani pamoja kisha kusaka uongozi katika maeneo mengine.

Umoja wa Pwani ni jambo ambalo bado ni vigumu utimie kutokana na uhusiano mbaya wa kisiasa ambao umechipuka kati ya Bw Joho na magavana Amason Kingi (Kilifi) na Salim Mvurya wa Kwale.

Uchaguzi mdogo wa Msambweni ambapo mwaniaji wa ODM Omar Iddi Bogo alibwagwa na Feisal Bader aliyekuwa akiungwa mkono na Bw Mvurya inaonyesha kuwa kutimiza ajenda ya umoja wa Wapwani bado ni kibarua kigumu.

Pia huko huko Pwani, Bw Odinga si mchache huku ODM ikijivunia umaarufu mkubwa na wengi wanamwona waziri huyo mkuu wa zamani kama mwokozi wao kuhusu masuala ya ardhi na dhuluma za kihistoria.

Kwa hivyo, huenda Mabw Joho na Oparanya wanamsindikiza Bw Odinga tu japo ukweli ni kwamba bado hawawezi kumpiku katika kusaka mchujo wa chama.

You can share this post!

TAHARIRI: Watoto walioacha shule watafutwe

WANGARI: Serikali ihakikishe kuna oksijeni ya kutosha...