• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
ONYANGO: IEBC ielekeze jinsi ya kuendesha kampeni za ugavana wa Nairobi

ONYANGO: IEBC ielekeze jinsi ya kuendesha kampeni za ugavana wa Nairobi

Na LEONARD ONYANGO

KIVUMBI cha kisiasa kilichotarajiwa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ugavana wa Nairobi utakaofanyika mwezi ujao huenda kikakosa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku mikutano ya kisiasa kwa siku 60.

Jumapili, Rais Kenyatta alisitisha mikutano ya kisiasa kando ya barabara au katika kumbi kama njia mojawapo ya kupunguza maambukizi ya virusi vya corona wakati huu ambapo shule zimefunguliwa.

Rais aliruhusu watu 150 tu kuhudhuria harusi au hafla za mazishi ambao watatakiwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na wizara ya Afya; kama vile kuvalia barakoa na kutokaribiana.

Uchaguzi mdogo wa ugavana utafanyika Februari 18 kabla ya kukamilika kwa marufuku hiyo ya siku 60.

Hiyo inamaanisha kuwa wawaniaji wa ugavana watalazimika kutumia mbinu mbadala kufikia wapigakura kampeni zitakapong’oa nanga kati ya Januari 18 na Februari 15, mwaka huu.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inafaa kushirikiana na wizara ya Afya kutoa mwongozo kuhusu namna kampeni zitaendeshwa.

Kupitia barua yake kwa Rais Kenyatta, Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata alionya kuwa mwaniaji wa chama cha Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Nairobi huenda akabwagwa.

Kulingana na Bw Kang’ata, chama cha Jubilee kimepoteza umaarufu nchini, likiwemo eneo la Mlima Kenya, na kushindwa kwa mwaniaji wake kutaleta aibu na litakuwa pigo kwa mipango ya maendeleo ya serikali bungeni.

Je, barua hiyo ya Bw Kang’ata ndiyo ilisababisha rais kupiga marufuku mikutano ya kisiasa nchini?

Ikiwa marufuku hiyo ina sababu za kisiasa basi IEBC haina budi kuingilia kati na kuhakikisha kuwa kila mwaniaji wa ugavana wa Nairobi atakuwa na nafasi sawa ya kufikia wapigakura.

Miezi michache iliyopita tuliona wanasiasa wanaounga mkono Naibu wa Rais William Ruto, maarufu Tangatanga, wakitawanywa kwa vitoa machozi kutokana na kisingizio kwamba walifanya mikutano ya kisiasa kinyume na masharti ya wizara ya Afya yaliyolenga kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

Wanasiasa wanaounga mkono handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, kwa upande mwingine, walifanya mikutano bila kuhangaishwa na maafisa wa usalama.

Katika nchi jirani ya Uganda, Rais Yoweri Museveni amekuwa akitumia kisingizio cha corona kukandamiza wawaniaji wa urais wa upinzani, haswa Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ambaye amekuwa akizuiliwa kufanya mikutano ya kisiasa ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Wakati huo huo, Rais Museveni amekuwa akikutana na makundi mbalimbali ya watu bila kuhangaishwa na maafisa wa usalama.

Rais Museveni amekuwa akiwafikia wapigakura kupitia vituo vya redio na runinga huku Bobi Wine akiachwa kutumia mitandao ya kijamii.

Tume ya IEBC iweke mikakati ya kuhakikisha kwamba mbinu hiyo chafu haitumiki katika uchaguzi mdogo wa Nairobi.

Janga la virusi vya corona lisitumiwe kukandamiza demokrasia.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: SGR iwape abiria huduma kisiwani

Barua kwa Rais: Kang’ata aomba msamaha