• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
ONYANGO: Serikali iongeze kasi ya utoaji chanjo ya corona

ONYANGO: Serikali iongeze kasi ya utoaji chanjo ya corona

Na LEONARD ONYANGO

HUKU Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022 ukikaribia, shughuli za kisiasa zinatarajiwa kuongezeka katika miezi ya karibuni na kuna hofu kuwa maambukizi ya virusi vya corona yataongezeka na kasi ya utoaji wa chanjo itapungua.

Magavana ambao wanasimamia afya katika kaunti, kwa mfano, watakuwa wakizunguka kila mahali wakitafuta kuchaguliwa tena huku baadhi ya maafisa wakuu katika wizara ya Afya wakijiuzulu kuenda kuwania nyadhifa za kisiasa.

Kampeni za siasa huenda zikasababisha Kenya kukosa kuafikia lengo lake la kutaka kutoa chanjo kwa watu milioni 15.8 kufikia Juni 2023 iwapo serikali haitaweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa shughuli za kisiasa hazilemazi utoaji wa chanjo.

Serikali ililenga kutoa chanjo kwa watu milioni 1.12 kati ya Machi na Juni, mwaka huu, na watu milioni 9.76 kati ya mwezi ujao na Julai 2022.

Ukweli ni kwamba tayari kasi ya utoaji wa chanjo ya corona humu nchini iko chini ikilinganishwa na mataifa mengine, na kukurukakara za kisiasa huenda zikachelewesha zaidi Wakenya kupata chanjo dhidi ya corona.

Tangu serikali ilipoanza kutoa chanjo ya AstraZeneca mnamo Machi, mwaka huu, ni takribani watu 980,000 ambao wamejitokeza kupewa chanjo, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya.

Hiyo inamaanisha kuwa dozi zaidi ya 120,000 hazijatumika kufikia sasa.

Watu wa umri wa miaka 58 na zaidi waliochanjwa ni 294,500 kufikia jana. Wahudumu wa afya ambao tayari wamepewa dozi ya kwanza ya Astrazeneca ni 165,600, walimu 152,000, maafisa wa usalama 82,000 na Wakenya wengineo 275,800.

Wahudumu wa Afya

Serikali ililenga kutoa chanjo kwa wahudumu wa afya 450,000. Hii inamaanisha kuwa wahudumu wa afya 280,000 hawajachanjwa licha ya kuwa katika hatari zaidi ya kuambukizwa virusi vya corona.

Idadi ya chini ya wahudumu wa afya wanaojitokeza kupewa chanjo ya AstraZeneca inatia wasiwasi.

Hii ni kwa sababu mbali na wahudumu wa afya kuwa katika hatari zaidi, wanachangia kwa kiwango kikubwa maambukizi ya virusi vya corona, haswa miongoni mwa wagonjwa ambao wanafika hospitalini kutafuta huduma za afya.

Wizara ya Afya inastahili kuanzisha kampeni ya kuhamasisha wahudumu wa afya kupewa chanjo.

Takwimu za wizara zilizotolewa Jumanne, kwa mfano, zinaonyesha kuwa ni watu 281 tu waliochanjwa dhdi ya corona. Watu wanne wa umri wa miaka 58 na zaidi walipata chanjo hiyo, 234 walikuwa wahudumu wa afya, maafisa wa usalama 19 na wengineo 24.

Ikiwa serikali itaendelea na kasi hii, itachukua muda wa takribani miaka minne kutoa chanjo kwa watu milioni 15.8.

Maambukizi ya virusi vya corona pia yanatarajiwa kuongezeka wakati wa kampeni za kisiasa mwaka ujao – kumaanisha kwamba idadi ya wagonjwa watakaohitaji kulazwa hospitalini itaongezeka.

Serikali inafaa ianze kujiandaa sasa kuhakikisha kuwa kampeni za 2022 hazitasababisha ongezeko la maambukizi ya corona na kutatiza utoaji wa chanjo.

You can share this post!

Mwanamke afa kwa ‘hofu ya kukamatwa na polisi’ Kilifi

KINYUA BIN KING’ORI: Maendeleo yasitolewe kwa...