• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
AMINI USIAMINI: Jinsi bodaboda wa kiume wanavyobakwa na wateja wao wa kike jijini

AMINI USIAMINI: Jinsi bodaboda wa kiume wanavyobakwa na wateja wao wa kike jijini

NA FRIDAH OKACHI

KATIKA harakati za kujitafutia riziki, wahudumu wa bodaboda nchini hukutana na wateja wa kila aina.

Mhudumu mmoja wa bodaboda katika eneo la Kangemi jijini Nairobi, anasimulia masaibu yake, akisema amewahi kubakwa si mara moja au mbili, lakini mara nne.

Anasema alisusia kuripoti dhuluma hizi kwa kuhofia kwamba wabakaji huenda wakabadilisha taarifa.

“Unapatana na mteja wa kike akiwa amenunua kiti au kabati na anataka umbebe na pia ufikishe mzigo hadi kwenye orofa anakoishi. Mkifika anakuambia hawezi akabeba peke yake. Unamsaidia kuweka kwa nyumba. Ghafla ajenda inabadilika. Katika kisa kimoja, nilipeleka kabati kwa nyumba ya mteja na papo hapo akafunga mlango na kunilazimisha nifanye mapenzi naye,” anasema mhudumu huyo.

Yeye ni baba wa watoto wanne na anasema anaona ugumu kuripoti visa hivyo kwenye kituo cha polisi kwa sababu anahofia huenda mambo yakabadilika na kugeuziwa kibao.

Hata anasema polisi wanaweza wakamcheka badala ya kumsaidia.

“Ninasita kujitokeza kuwa nimebakwa. Hapa nchini maafisa wa polisi hawawezi wakaamini. Kitu kingine jamii haiwezi kukubali kwamba nimebakwa. Mambo yatapinduliwa kwa kuwa watu watauliza mwanamke anakubaka aje?” anasimulia.

Taifa Leo pia ilimpata mhudumu mwingine wa Kawangware jijini Nairobi ambaye ana masaibu sawa na mwenzake wa Kangemi. Yeye naye anasema mteja wake fulani amekuwa akimuwinda kwa kipindi cha zaidi ya miezi saba. Siku moja mteja wake huyo wa muda mrefu alifunga mlango na kumtishia kwamba angepiga kelele kama mhudumu huyo angekataa kufanya tendo hilo alilotaka.

“Nilifika kwa nyumba na nikatua mzigo wa mteja wangu lakini kabla sijaondoka, mteja wangu alifunga mlango. Kidogo nikamuona mteja wangu akiwa hana mavazi. Nilijaribu kadri ya uwezo wangu kujitetea, akanitisha atapiga kelele,” akasimulia bodaboda huyo.

Afisa wa haki ya afya na uzazi Bi Elsie Milimu kutoka shirika la Kelin anasema unyanyapaa na itikadi za kijamii zinazuia watu wa jinsia ya kiume kujitokeza kushtaki dhuluma za aina hii.

“Kuna huo uoga wa kushtaki. Sheria haibagui ikiwa wewe ni mwanamume au mwanamke. Katika vituo vya polisi kuna tashwishi. Wanahisi kuwa wataulizwa mwanamke anakubaka aje,” alisema Bi Elsie.

Ubakaji hauathiri wanawake pekee.

Pia wanaumme wanadhulumiwa na kunyanyaswa kimapenzi.

Utafiti unaonyesha kuwa asilimia saba ya wanaume hubakwa hapa nchini Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Aisha Jumwa apiga abautani na kukataa disko matanga...

Waziri Soipan Tuya aomba mahakama iagize mume wake kutoa...

T L