• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Aisha Jumwa apiga abautani na kukataa disko matanga alizowahi kushabikia

Aisha Jumwa apiga abautani na kukataa disko matanga alizowahi kushabikia

NA MAUREEN ONGALA

WAZIRI wa Jinsia Aisha Jumwa amebadilisha msimamo wake kuhusu disko matanga katika Kaunti ya Kilifi.

Akihutubu kwenye mazishi ya aliyekuwa mwanahabari wa kituo cha redio cha Pwani FM Sammy Ambari, waziri huyo alisema kuwa disko matanga zimechangia pakubwa kuongezeka kwa visa vya dhuluma za kijinsia na mimba za mapema miongoni mwa wasichana wa shule katika kaunti hiyo.

Amebadili msimamo wake wa awali ambapo Bi Jumwa alikuwa ametangaza kuwa disko matanga Kaunti ya Kilifi ziruhusiwe. Awali alikuwa ameonya viongozi wa utawala na polisi dhidi ya kuhangaisha wananchi walioendeleza disko matanga, akiwataka badala yake kuwatia mbaroni watoto ambao wangepatikana kwenye disko pamoja na wazazi wao na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Bi Jumwa alikuwa amesema hayo mwaka 2022 wakati wa kuanzishwa rasmi kwa maadhimisho ya siku 16 za kutetea haki za binadamu katika uwanja wa Water mjini Kilifi, miezi michache baada ya kutawazwa kuwa Waziri wa Jinsia.

Wakati huo alidai kuwa marufuku ya disko matanga yalikosa kuzaa matunda ya vita dhidi ya mimba za mapema katika Kaunti ya Kilifi na yalikuwa yanawanyima wamiliki wa vyombo pato lao la kila siku.

Lakini akihutubia waombolezaji wa mwanahabari aliyejitia kitanzi, Bi Jumwa alipiga marufuku disko matanga na kutaka Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro na kamishina wa Kilifi Josephat Biwott kufuatilia kwa ukaribu agizo hilo.

“Wakati mimba za mapema zilikuwa nyingi Kilifi, tuliambiwa kwamba sababu kubwa ni vijana wa bodaboda, umaskini na disko matanga kwa upande mmoja, lakini sikukubaliana na walioshikilia msimamo huo wakati huo,” akasema.

Alisema Rais William Ruto ameunda jopo la kuangalia tatizo la mimba za mapema nchini na anaendeleza kampeni ya kusitisha mimba hizo.

“Kama viongozi tutafunga kila njia ambayo inatuelekeza kwa changamoto ya mimba za mapema… na ya kwanza ni disko matanga,” akasema.

Aidha waziri alisimulia kero aliyokumbana nayo kwa siku tatu wiki tatu zilizopita alipokuwa nyumbani kwake Kakuyuni katika eneo bunge la Malindi.

“Nilipokuwa pale nyumbani, nilisikia ngoma inapiga hapa na pale na iliendelea mpaka saa kumi na mbili asubuhi. Unaskia kelele unajifunika na takia (pillow) lakini wapi… huku ngoma ikiendelea kurindima,” akasema.

Waziri Jumwa alieleza kuwa alimtumia kamishina wa kaunti ya Kilifi Bw Biwott ujumbe mkali.

“Nilimwambia kamishna wa Kilifi kuwa kutoka hiyo siku kuendelea hakuna disko matanga zitaruhusiwa kucheza kutoka saa kumi na mbili jioni hadi asubuhi. Hatuwezi kukubali kama viongozi wa kutoka Kilifi,” akasema.

Aliwauliza wakazi maswali na kutaka kujua kama hakuna binadamu ambaye atachoka kwa kukesha akicheza.

Alisema jamii imekosa kucheza nyimbo za kitamaduni kama ilivyokuwa desturi na wanacheza nyimbo za kisasa tena za kidunia zinazopotosha.

“Watoto wetu wanahangaika, sisi wenyewe tumechoka na dunia na tunataka kupumzika lakini haiwezekani kwa sababu ya disko matanga,” akasema.

Jumwa alitaka serikali ya kitaifa na ya kaunti kuhakikisha kuna mipangilio maalum wakati familia ya mwenda zake inapotaka kufanya mchango kwa ajili ya kukusanya pesa za kuifaa kuendesha mipango ya mazishi.

“Inashangaza sana kuwa familia zinachanga pesa kutokea saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi. Je, watu wanatoa wapi pesa za kuchanga muda huo wote?” akauliza waziri Jumwa.

Alisema michango itasurusiwa kutoka saa kumi na mbili jioni hadi saa nne usiku pekee.

“Ni lazima watu wawe na nidhamu. Tunaelekea likizo na hatujui tutawaficha wapi watoto wetu kwa sababu watatoroka majumbani na kujihusisha na ngono na mambo mengine yasiyofaa kwa watoto,” akasema.

Aliwataka wenye vyombo vya kucheza disko kuwa na mipangilio wakati wanapofanya shughuli zao.

Aliyekuwa Waziri wa Usalama na Maswala ya Ndani Dkt Fred Matiangi alipiga marufuku disko matanga katika Kaunti ya Kilifi kwa kuchangia uhalifu na mimba za mapema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mzozo wapasua Kanisa la African Divine Church katikati

AMINI USIAMINI: Jinsi bodaboda wa kiume wanavyobakwa na...

T L